Friday, January 25, 2008

Ufisadi BoT: Ballali hatosema lolote

Mpira umekwisha.

Ballali amekuwa mbuzi wa kafara. Sidhani wala sitegemei kuwa Ballali atasema chochote. Aseme nini? Naye kibarua chake "kimetenguliwa?" Tusubiri tuone.

TABIA YA KUTELEKEZA

Nimevutiwa sana na picha ya lori lililotekelezwa huko Kantalamba Sec.School. Picha hiyo inaonekana kwenye blog ya Mjengwa.

Ndiyo, ugonjwa wa kutelekeza ni mkubwa sana kwenye jamii yetu. Umekuzwa hadi kwenye taasisi zetu za serikali ambako umeota mizizi. Gari jipya linaweza kutelekezwa kwa kukosa kipuri cha Tshs 20,000/=, kompyuta ya miezi 2 inaweza kutlekezwa kwa kukosa cartridge, pikipiki kwa kukosa tairi n.k.n.k. Eti taasisi imekosa fedha hizo.

Maggid, kuna vingi vimetelekezwa kwenye taasisi zetu na kama itafanyika "study" basi mioyo yetu itasimama jinsi raslimali zetu zinavyotelekezwa.

AMEUNGUZWA NA KURUKIA DALADALA

Siku ya Jumanne wiki hii, pale Mbagala Rangi 3 lilitokea tukio la ajabu.

Kuna kibaka alibambwa, akapigwa na kuchomwa moto.Lakini kwa maajabu ya mwenyezi Mungu, moto ulipozimika aliweza kunyanyuka na kutembea.

Asubuhi hiyo ya Jumanne nilimshuhudia mtuhumiwa huyo akitembea kama sanamu vile! Huku wananchi wakimzonga na kumzomea. Ee bwana eeh, alikuwa kama mzuka vile, maana ngozi ilianza kubanduka na kuonyesha ile rangi ya ndani nyeupee! Huwezi kutazama mara mbili nakwambia. Damu ilikuwa inamtirirka kichwani hadi mdomoni, nakwambia hata kama alikuwa ndugu yako usingeweza kumtambua. Nguo zilionekana ni matambaratambara na amevikwa upati kuhifadhi sehemu nyeti. Alhamdulilah!. Lakini cha kushangaza, kipande cha baba kile kwa ghafla na bila kutarajia aliweza kudandia daladala ya Ubungo huku akituacha hoi .

Habari nilizozipata baadaye ni kwamba kibaka huyo alimalizwa na wananchi wenye hasira hadi kufa!

Vibaka acheni ukwapukwapu mtapoteza maisha hivi hivi. Wananchi wema wamechoka na vitendo vyenu. Nguvu mnazo zitumieni kwa kufanya kazi halali.

Wednesday, January 23, 2008

TABORA MJI MSAFI

Mwezi Desemba mwaka jana (2007) nilikuwa mjini Tabora. Mimi si mgeni sana wa mji wa Tabora, nimeshatembelea Tabora karibu mara tano sasa. Lakini mwaka jana nilifurahishwa na hali ya usafi wa mitaa ya mjii wa Tabora.

Barabara zimefagiliwa, mitaro imezibuliwa na ni nadra sana kukuta lundo la taka kando ya barabara.

Nilipowauliza wenyeji, siri ya usafi wa mji wa Tabora, wengi walisema kuwa ,shughuli ya usafi katika mji huo ni shirikishi. Unaanzia kwenye kaya. Kila mwana kaya anawajibika, viongozi wa mtaa wanawajibika na Halmashauri nayo inawajibika. "Siku nyingine uchafu unazolewa mara mbili kwa siku."Anasema mkazi mmoja wa mji wa Tabora.

Si kwamba Tabora wana magari mengi ya kusomba uchafu. Kwanza sikuyaona magari hayo. Lakini wamejipanga.

Mjini Tabora huwezi kuona vibanda vya ovyo ovyo. Shughuli za biashara ziko sehemu zilizopangwa. Hata pale sokoni Tabora kuna mpangilio kuna sehemu za biashara ya kuku na nyingine za "Music Systems, TV, n.k."

Iiiiii kwa usafi mmewashinda watani zenu wa Morogoro. Mmewakandamiza kabisa! Tujage mwanawane. Manispaa Morogoro tumeni ujumbe Tabora mkajifunze usafi kidogo.

Lakini nimedokezwa kuwa Musoma ni kiboko ya usafi. Nitafika huko siku moja na "nitawakandamizia" ya huko kwenye blog hii.

Napendekeza uwepo ushindani wa usafi kwa miji yetu. Na washindi wapewe zawadi za kuiweka miji hiyo katika hali nadhifu.

Ni waulize swali.

"Ni kweli hatuwezi kutengeza ndege, usafi je?"

JIJI LA DAR BADO CHAFU!

Mwaka mpya wa 2008 ndo umeshaanza na siku 22 zimeshakatika. Lakini Dar bado chafu! Dar bado ni ile ile ya mwaka 2007. Nimetembelea Kinondoni-chafu, Ilala- chafu na Temeke - chafu!

Mitaro imeziba, malundo ya taka yamezagaa barabarani. Nzi wanaruka ruka kwenye mabaa, migahawa na mitaani.

Dar unaweza ukajibanza pembezoni mwa barabara na kukojoa bila woga. Akukamate nani ? Huo ndo ustaarabu wetu na mgambo wa jiji akifanya hivyo anaambiwa noma mshikaji.

Siyo kusema kuwa sheria hakuna la hasha, zipo (Nitauliza viongozi wa jiji adhabu ya kukojoa ovyo jijini) ila utekelezaji wake ni wakishikaji. Mgambo wa "jiji" anaweza kukamata lakini ukimwachia shilingi 200 anakuachia, huku ukiwa umeacha uchafu na pengine ugonjwa! Tunauza ugonjwa kwa shilingi 200!

Tabia hii ya uchafu ipo ndani ya jamii zetu, nyumba zetu na ofisi zetu na wala hatujali. Hatuna maadili mema ya usafi. Hatutaki kuwafundisha watoto wetu usafi. Kwamba kutupa taka ovyo ni uchafu na ni tabia mbaya. Hatufanyi hivyo.

Kweli inatupasa kujipanga upya JIJI LETU KUBWA LA DAR BADO NI CHAFU!

Johnson Mbwambo ulichoandika ni sahihi

Moja ya makala yangu ya hivi karibuni katika blog hii ilikuwa ni kulikaribisha gazeti la Rai Mwema nikasema karibu mgeni wetu.

Mgeni huyu kwa kweli anafanya mambo mengi. Anafagia nyumba, anaosha vyombo baada ya kula chakula wakati mwingine anakwenda shamba na kubeba mizigo! Kweli mgeni njoo mwenyeji apone!

Moja ya toleo la Raia Mwema, mwandishi wake mahili Bw. Johnson Mbwambo aliandika kuhusu uamuzi wa kujenga kiwanda cha Magadi kwenye eneo la ziwa Natron. Mbwambo ameandika mengi kuhusu hasara itakayopatikana kimazingira kwa uamuzi huo hasa kusumbua viumbe hai (Ndege na wanyama) waliopo kwenye maeneo hayo. Aliwataja ndege aina ya Flamingo ambao ni adimu hapa duniani na wanapatikana kwa wingi hapa Tanzania. Watalii wengi huja kuwaona ndege hao na kwa kufanya hivyo huongeza pato la taifa.

Pamoja na athari nyingine nyingi kimazingira lakini wakubwa wameshakilia uamuzi wao wa kujenga kiwanda hicho ambacho inaonekana hakitakuwa endelevu wao wameshikilia kuwa kitatoa ajira kwa wingi. Sawa, lakini je ajira hizo ni endelevu? Au ndo mtu kishachukuwa chake kabisa?

Johnson ameandika, sisi tumekusoma. Raia Mwema atakuwa shahidi. Tusubiri tuone!

KALAVATI MIEZI MINNE?

Kwa mkazi wa wilaya ya Temeke, au kwa yeyote yule aliyekwisha fika Tandika kwa kupitia Sokota anaifahamu sehemu korofi pale kwenye kituo cha mafuta - Sokota unapoacha barabara ya Mandela na kuingia Sokota kuelekea Kituo cha Polisi Chang'ombe.

Nasema korofi kwa nini? Mvua ikinyesha kidogo tu basi maji kibao, maji yakikauka huacha korongo kubwa. Ukarabati wa kibabaishaji umekuwa ukifanyika mara kwa mara. Mara wamwage kifusi- ambacho hugeuka tope mara wafanye hivi lakini haikusaidia. Shida, karaha wakati wote na wakati mwingine uharibifu huu wa barabara umekuwa ukisababisha ajali zisizo za lazima.

Mkandarasi amepatikana tokea mwaka jana kujenga "culvert" au kwa lugha ya kawaida ya mtaani kalavati (mtaro wa maji chini ya ardhi). Cha kushangaza mtaro huu umechukua miezi minne kukamilika. Jamani, kalavati moja tu hilo, miezi 4 sasa kweli huo ndiyo uwajibikaji? Kwa miezi 4 usafiri kupitia sehemu hiyo ulikuwa umefungwa, fikiria mwenyewe usumbufu karaha na mambo mengine. Kweli kwa mtindo huu Watanzania tutafika? Tena zabuni hiyo amepewa mzalendo. Kujenga kalavati moja miezi 4? Akinyimwa oh hatuna uzalendo. Mimi ninachojali bwana huduma safi mtu apewe kazi kutegemea uwezo siyo kubebana bebana hapa tumechoka na hali hii. BoT wabebane hata kwenye kalavati?

ASANTE WASOMAJI WA BLOG-Banzi wa Moro

Nimepata maoni ya wasomaji wa blog hii- Pets na Belo asante sana kwa maoni yenu. Kwani yameniongeza nguvu mpya. Kuna mmoja amekuja na takwimu kabisaa! Mwaka 2006 nimeandika makala 16, mwaka 2007 , 16 tena bila kufumba macho akasema kweli nilikuwa mvivu. Hata mimi nimeliona hilo. Ndo maana nimejiwekea malengo kwa mwaka 2008 (100).


Asanteni sana

Monday, January 14, 2008

WENGI HAWAIFAHAMU ASDP

Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo iliyozinduliwa mwaka wa fedha 2006/07 inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Kilimo.

Kwa kweli hata serikali ya awamu ya NNE chini ya uongozi wa Mh.Rais Jakaya Kikwete inaitegmea Programu hii kuboresha maisha ya wakulima wetu huko vijijini. Pamoja na matumaini makubwa waliyonayo hasa viongozi wa ngazi za juu, napenda kutoa maoni yangu kuwa wananchi wengi bado hawafahamu utekelezaji wa programu hii. Hii inathibitishwa na jinsi fedha zilizotumwa kwenye Halmashauri nyingi zinapokosa kazi.

Nilikuwa na mazungumzo yasiyo rasmi na mmoja wa wakuu wa wilaya hapa nchini. Alinieleza bila kuficha kuwa hata yeye hafahamu vizuri. Tatizo ni kwamba utendaji katika ngazi ya Halmashauri hauko wazi kwenye utekelezaji wa Programu hii ambako asilimia 75 ya fedha za programu hii hutumwa huko.

Kama hali ndiyo hii. Kwa kweli tuna kazi ya kufanya, ni lazima tupitie programu hii kwa haraka sana na tubadilike katika utendaji wa kutekeleza programu hii. Nina wasiwasi muda uliopangwa wa utekelezaji wa programu utapita na matokeo yasiwe mazuri. Hii ni lugha rahisi sana. Lakini ni hatari kwa maendeleo ya sekta hii.Tutambue hilo na ndo ukweli wenyewe.

MORO WAWAAA

Ndiyo, lazima ufagie nyumbani kwanza. Mwaka mpya unaanza kwa matambiko bwana! Mimi ni Banzi wa Moro maji yatiririka milimani!
Ni kweli hivi karibuni nilikuwa pale Moro mjini, kikazi. Lazima niseme.
Kitu kilichonifurahisha ni jinsi MANISPAA inavyotunza ile mizunguko ya kupita KUSHOTO iliyopo barabarani pale mjini (KEEP LEFTS). Kwanza kuna mzunguko mkubwa kabisa pale MSAMVU, bustani ya maua ni safi na kijana yule anayehudumia pale kwa kweli anachapa kazi.Bustani ile inavutia.

Unakuja hapa MASIKA napo wawaaaa na kibao kimesimikwa USITUPE TAKATAKA na kweli hakuna TAKA.

Unashuka pale stendi ya zamani. Kwenye kituo cha Mabasi ya Kwenda MATOMBO bustani safiii. Kijani kibichi kabisaa na ukiangalia milimani nako maji yatiririka basi raha mpaka kisogoni. Sawa, ukienda Posta karibu na NBC bustani nzuri imetunzwa vizuri. Basi hiyo ndiyo mandhari ya Moro mji kasoro bahari na kiswahili chetu cha kuimba, Utatupenda! Jamani!

Angalizo kwa Uongozi wa Manispaa
  • Kituo cha mabasi cha Msamvu inabidi kuboreshwa zaidi, wakati wa mvua na jua ni shida tupu.
  • Soko kuu la mjini pale Kikundi linataka ubunifu zaidi. Watu wanaongezeka bidhaa zinaongezeka na mahitaji yanaongezeka.
  • Barabara ya kwenda Kilakala Sekondari iwekwe lami

Vinginevyo Moro wawaaa, mashindano ya Abood Bus naHood ni burudani tosha ukiwa pale Msamvu!

MWAKA 2007 NI HISTORIA, 2008 UTAKUWAJE?

Heri ya mwaka mpya wasomaji wa Blog hii. Mwaka 2007 ulikuwa na mambo mengi vituko vingi, bashasha nyingi, kashkash au mitikasi mingi kama mdogo wangu Kamsopi anavyozoza.
Hata hivyo namshukuru Mungu kwa kunilinda na kunipa afya ya kutosha kuweza kutekeleza majukumu yangu kwa mwaka mzima na kikubwa ni kuniwezesha kupata MKATE wetu wa kila siku mimi na familia yangu kama tunavyoomba siku zote.

Kweli nimekuwa mvivu sana kuandika kwenye blog yangu kwa kipindi cha mwaka 2007. Pengine hii ndiyo ile hali tuliyonayo waswahili wengi, nitafanya kesho, kesho, hadi mwaka unakatika. Baadaye miaka 60 inafika tayari umeshafungwa goli la lala salama. Ulikuwa na mipango ya kujenga nyumba 3. Moja Dar, nyingine Morogoro mjini na nyingine kijijini Matombo lakini unashtuka umejenga nyumba 0 hayo yamewakuta wengi tu.

Jamani eeh, sasa mimi naahidi kupunguza uvivu angalau makala za mwaka huu ziongezeke. Lengo MAKALA 100. Mmenipata? Eeh ndiyo hivyo tena lazima kuwa na malengo, vinginevyo nI uswahili uswahili tu. Na utanipimaje? Siyo UTANITAMBUAJE ya Beny Mwaitege. Chati siyo huyo mwalafyale?

Karibu mgeni wetu 2008. Sijui ulikotoka, lakini karibu duniani. Hapa umeyakuta na utayaona mengi. Tuvumilie mgeni wetu. Lengo la mwaka huu nimeshalitaja hapo juu. Tushirikiane na naomba mnipatie maoni yenu wasomaji wangu ili nami nipate moyo wa kuandika!

"HAPPY NEW YEAR"