Friday, May 23, 2008

Tutafakari Mei Mosi




Kila mwaka ifikapo tarehe 1 Mei Wafanyakazi dunia nzima husherehekea sikukuu ya wafanyakazi. Kwa kulitambua hili Tanzania huwa inaadhimisha sikukuu ya wafanyakazi kwa maandamano, hotuba, michezo na maonyesho ya wafanyakazi. Sare za kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi kama vile TUGHE, RAAWU havaliwa siku hiyo.




Nimekuwa nikijiuliza mara kwa mara hivi wafanyakazi huwa tunasherehekea nini ikiwa yale tunayohitaji mara nyingi huwa hayatimizwi, ahadi zinazotolewa huwa hazitimizwi.




Hivi kweli wafanyakazi huwa tunajipima kila mwaka kuwa tumetoa mchango gani katika ujenzi wa Taifa? Umetoa mchango gani katika maendeleo ya familia yako? Je, inakusaidia? watotot wa mjini wanasema inalipa? Inakuletea heshima na raha? Unajisikiaje unapoamka asubuhi na kwenda kazini. Unafahamu unachokwenda kufanya? Una ratiba ya kazi? Bosi wako na wafanyakazi wengine mnashirikianaje katika kukamilisha malengo?






Wengi hatujiulizi maswali hayo ya msingi, miaka nenda miaka rudi mambo ni yale yale tu. Wengi wetu tunafikiri Mei Mosi ni siku ya kupata sare kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi.




Tutafakari MEI MOSI!

Tuesday, May 20, 2008

Padri Jakka "awabangulila" Wakristu wa Matombo

Paroko wa Parokia ya Kidatu, jimbo la Morogoro, Padri Venance Jakka "amewabangulila" (amewapasha) wakristu wa Matombo kuacha imani za kishirikina na kumkiri Kristu na kufuata imani yao badala ya kuendekeza ushirikina ambao unaonekana kusambaa kwa kasi ya ajabu. Padri Jakka aliyasema hayo tarehe 12 Mei kupitia mahubiri yake aliyoyatoa wakati akimzika baba yake marehemu Mwl. Ephrem Ephrem Mbiki kijijini Nige, Kariakoo-Matombo.

Fr.Jakka alisema kuwa Kanisa Katoliki Matombo ni kanisa Mama katika jimbo la Morogoro Ukristo una historia ndefu Matombo kwa hiyo lisichezewe. Anashangaa kuona Wakristo wa Matombo wamebadilika na kuamini mambo ya kishirikina. Watu wanadanganywa na waganga kuwa wanatoa majini na vitu vingine. " Ni uongo, wanawadanganya, wanawalia pesa zenu nanyi mnabakia kuwa masikini. Nashangaa kuona mtu yuko tayari kuchangia fedha kumuita mganga wakati anashindwa kula vizuri, kuvaa vizuri na kuishi kwenye nyumba bora." Alilalamika Padri. Jakka. Aliongeza kwa kusema kuwa mtu utaachaje kuugua kama huogi, huli vizuri, unaendekeza pombe! Utawezaje kuwa na afya nzuri? Aliuliza.

Aliwasihi wakristu wa Matombo kuacha tabia ya kuendekeza ushirikina na kumrudia Mungu wetu. Alisisitiza kwa kusema kuwa tukio la leo litukumbushe kitu kimoja kuwa, kila mmoja wetu atakufa. Kwa njia ipi hiyo haifahamiki. Ni kweli kila mmoja wetu anaogopa kufa lakini lazima tufe. Kwa hiyo basi inatubidi tujitayarishe kwa kuishi maisha mema wakati wote.

DAR, ARUSHA, MBEYA-BADO

Mwezi Mei mwaka huu nimepata kuishi kwenye majiji yetu matatu ya hapa Tanzania:- Dar Es Salaam, Arusha na Mbeya. Ukweli ni kwamba pamoja na kuitwa majiji lakini viwango vyake bado ni vya chini ukilinganisha na majiji ya nchi nyingine nilizotembelea.

Kwanza majiji yote matatu ni machafu kwa mazingira. Karatasi zimezagaa hovyo, mitaro ya maji machafu, imeziba taka zimelundikana mitaani. Nilishangaa kuona hali hiyo ipo hata Arusha. Zamani Arusha ilikuwa ikisifika kwa usafi wake lakini sasa hakuna kitu. Arusha ina nuka! Ni shida kupata vyoo vya kujisadia ukiwa mjini itabidi uzunguke sana.

Na hapa Dar ndo kabisa balaa. Siku moja asubuhi nilikuwa nikisafiri kwenda Morogoro,wakati nilipokaribia kituo cha mabasi pale Ubungo nilikuta kinyesi cha mwanadamu kando ya barabara, aibu kabisa!

Mbeya nako, ushirikina hadi jijini. Asubhi na mapema, watu wanakwenda kazini pale airport -Mwanjelwa kichwa cha mbuzi kimewekwa kwenye makutano ya barabara! Jiji hilo!

Barabara za majiji yote hayo ni mbaya! Kwa mfano barabara nzuri pale Arusha pengine ni tatu tu nyingine hovyo kabisa. Mbeya 2 tu. Nyingine za mwaka 47. Hivi tuna mikakati gani na majiji yetu. Hivi kweli Watanzania tuko "serious" kwa hili? Aaa wahusika acheni uswahili angalieni majiji yetu yanavyoendeshwa aibu!

MBAGALA HALI ILE ILE!

Mvua hizi za masika zinazokaribia kukatika zimewarudishia adha ya usafiri wakazi wa Mbagala ambayo walishaanza kusahau. Baada ya mvua kunyesha imeharibu sana barabara ya Kilwa hasa maeneo ya Mtongani hadi KTM na kuiacha katika mashimo makubwa wenywe wanayaita "mahandaki." Mashimo haya yanasababisha magari kupunguza mwendo na kuyakwepa mashimo hayo kutokana na hali hiyo kunakuwa na msongamano wa magari barabarani. Tatizo kubwa hapa kama nilivyokwisha eleza hapo juu ni mashimo.

Ninachojiuliza kuwa, Je, TANROADS wanasubiri mpaka mvua ikatike ndo waanze kukarabati barabara wakati watu wanateseka. Isitoshe wanapooanza kukarabati hurashia rashia tu ndiyo maana kila mvua inaponyeesha basi mashimo hutokea. Hii ndiyo hali halisi, si kweli kuwa Mbagala na vitongoji vyake ni vibaya na hazikaliki. Mbagala ni sehemu nzuri sana. Lakini barabara inawaangusha watu wa Mbagala. Kibaya zaidi kuna barabara moja tu ya kufika kati kati ya jiji.

MWL. EPHREM EPHREM MBIKI HATUNAYE TENA

MWL. EPHREM EPHREM MBIKI HATUNAYE TENA

Tarehe 10 Mei, 2008 saa 8 mchana –Jumamosi, ukoo wa Wambiki ulimpoteza mtu muhimu sana katika ukoo huo naye si mwingine bali marehemu Mwl.Ephrem Ehprem Mbiki.

Kumbukumbu za mama yake mdogo Sista Maria Magdalena (Bibi Constancia Makeya) zanaeleza kuwa Mwl. Ephrem , kama alivyojulikana na wengi alizaliwa mwaka 1932 kijijini Nige, Matombo, Morogoro. Mwl. alikuwa ni mtoto wa tano kutoka familia ya watoto 9 wa Mzee Ephrem Kobelo Lugongo na Bibi Fransickka Makeya (wote marehemu).

Alipata Elimu yake ya Msingi – Matombo Middle School na hatimaye kujiunga katika Chuo cha Ualimu Kigurunyembe ambako alihitimu mwaka 1953. Mwaka 1954 alifunga ndoa na Bi. Fortunata Epimark wa Kigurunyembe Morogoro.

Katika uhai wake alifundisha katika shule zifuatazo: – Msata (Bagamoyo), Misegese –Mlali (Morogoro vijijini), Gozo-Matombo (Morogoro vijijini) na hatimaye shule ya msingi Matombo (Morogoro vijijini) kwa mkataba baada ya kustaafu.

Mwl. Ephrem alibahatika kupata jumla ya watoto 17 ambao hadi sasa walio hai ni 13 pamoja na wajukuu kadhaa.

Wanaomfahamu Mwl. Ephrem akiwemo mdogo wake Emili Wendelini “Bongwa” wameeleza kuwa marehemu atakumbukwa kwa kuwa alikuwa mshauri mzuri katika familia na aliweza kuikusanya na kuitambua popote ilipo, kiongozi wa dini hasa katika kusimamia Jumuiya Ndogo Ndogo, mtulivu na asiye na hasira, na alikuwa tayari kukosolewa na kushauriwa. Lakini pia alikuwa ni mcheshi kwa wakubwa na watoto.

Kama Mwalimu, alikuwa mwalimu mzuri ambaye aliweza kuboresha shule zote alizopitia. Kwa mfano alipohamishiwa shule ya msingi Gozo, wakati huo shule hiyo ilikuwa hadi darasa la nne tu, lakini yeye alifanikiwa kuipandisha chati hadi kufikia darasa la saba. Shuleni Msata, alimfundisha Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa darasa la kwanza.

MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MWL. EPHREM MBIKI

Saturday, May 17, 2008

Moro-Matombo, barabara itengenezwe

Jumapili iliyopita nilisafiri kwenda kijijini kwetu Matombo-Morogoro kumzika baba yangu Mwl.Ephrem Ephrem Mbiki {Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.AMINA}.

Ni kilomita 65 kutoka Morogoro hadi Matombo (Nige-Kariakoo) lakini tulitumia masaa matatu na nusu. Tatizo barabara ni mbaya kwelikweli. Ubaya wa barabara unanzia Mkuyuni hasa sehemu za Mbehombeho na mlima wa Kibungo. Mashimo, mawe yaliyojitokeza barabarani na maji yanayotiririka na kuingia barabarani na kuharibu zaidi barabara. Pale Kibuno mlimani jiwe kuu liliporomoka na kuziba barabara. Ajabu katika kulipasua jiwe hilo bado teknolojia za zamani zinatumika kupasua kwa tindo!

Safari ya saa moja imetuchukua karibu masaa manne. Hii ni hatari sana. Ni hatari kwa maendeleo ya watu wa Matombo. Mamlaka husika haziwatendei haki wananchi wa Matombo. Wakulima wa Matombo ni wazalishaji wakubwa wa Matunda na mboga wanalisha kwa asilimia kubwa wakazi wa jiji la Dar Es Salaam, Morogoro, Dodoma hata Iringa. Yaonekana hakuna mipango madhubuti ya kuiweka barabara hiyo katika hali nzuri ya kuweza kupitika mwaka mzima. Matombo si maarufu kwa mazao ya kilimo tu. Madini ya aina mbalimbali yanapatikana Matombo. Kuna vivutio vya utalii katika mbuga ya Selous na milima ya Uluguru. Isitoshe mto wa Ruvu unaanzia kwenye milima ya Uluguru iliyoko Matombo. Tuamke na tuiboreshe barabara hiyo kwa manufaa ya watu wetu.

NAKUPA SHAVU MMILIKI WA MABUS YA SUMMRY

Hivi karibuni nilisafiri kwenda Mbeya kwa kutumia bus la Sumry. Kwa kweli huduma za mabus hayo ni nzuri kwa wakati tulionao sasa.

Kwanza wanajali muda. Pili mwendo si wa kasi tatu wahudumu wana lugha nzuri kwa wateja (wasafiri), nne mpango wao wa kutoa huduma ya vinywaji baridi na vichangamsha mdomo (pipi) vinakupa uhakika wa kutulia kwenye basi hata kama huna vijisenti vya kununulia chakula wakati ukisafiri. Isitoshe ukiwa ndani ya bus unapata muziki murua na picha za video.

Kwa hakika mabus ya Sumry yanafaa kwa usafiri kwa watu wa rika zote, watoto, vijana na wazee.Si shangai kuona kuwa sasa wamefunika kabisa kwa huduma za usafiri kanda za Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Rukwa, Iringa, Ruvuma).

Mara nyingi tumeona kampuni mbalimbali za usafiri zikianzishwa na kutoa huduma bab kubwa lakini baada ya muda huduma huzorota na kampuni hiyo kufa kabisa. Hebu tuangalie Scandavia inakoendea hivi sasa, choka mbaya! Sumry, isiwe ikawa "Mgema ukimsifia, tembo hulitia maji"

WANAWAKE - Wajasiriamali Arusha

Ukitaka kuona jinsi wanawake wanavyochacharika kutafuta maisha au kitu pesa basi nenda Arusha. Wanawake wa Arusha hawatulii. Biashara za mboga na matunda huko sokoni karibu asilimia 80 zinafanywa na wanawake. Leo asubhi nilikuwa nikipita pita kwenye baadhi ya mitaa ya Arusha nimewakuta wanawake wakiwa na malundo ya mitumba wamebeba kichwani na wengine wametandaza chini ni itumba ya kila aina. Soksi, mashati, suruali na makoti.

Pale kati kati ya mji sokoni, nilibahatika kununua sabuni nzuri sana ya mche ambayo inafaa kwa kufulia na kuogea (nafikiri zinatoka Kenya). Aliyeniuzia ni mwanamama tena kilema wa mguu.

Hawa ndo wanawake wa Arusha. Na usidhani unaweza kuwasumbua kwa "vijisenti" vyako kwani wanavyo tena viko hapahapa Tanzania! Hongera sana wanawake wa Arusha.

SIYO CHELSEA NI VODAFASTA-ARUSHA

Nipo Arusha yapata juma moja sasa. Moja ya vitu vilivyonishtua na kunifurahisha katika jiji la Arusha ni jinsi huduma ya VODAFASTA inavyopatikana karibu katika kila kona ya jiji. Ukitupa jicho kulia na kushoto mbele na nyuma hukosi kuona rangi nyeupe. Hao si wengine bali ni watoaji huduma wa VODAFASTA. Mwite, msimamishe popote pale huduma ya voda chapchap.

Huu ndiyo ushindani wa kibiashara ama kwa hakika naweza kusema VODA wamefanikiwa sana kwa jiji la Arusha. Huu ni ubunifu mzuri. Wateja tunafurahia huduma za aina hii.