Tuesday, May 20, 2008

Padri Jakka "awabangulila" Wakristu wa Matombo

Paroko wa Parokia ya Kidatu, jimbo la Morogoro, Padri Venance Jakka "amewabangulila" (amewapasha) wakristu wa Matombo kuacha imani za kishirikina na kumkiri Kristu na kufuata imani yao badala ya kuendekeza ushirikina ambao unaonekana kusambaa kwa kasi ya ajabu. Padri Jakka aliyasema hayo tarehe 12 Mei kupitia mahubiri yake aliyoyatoa wakati akimzika baba yake marehemu Mwl. Ephrem Ephrem Mbiki kijijini Nige, Kariakoo-Matombo.

Fr.Jakka alisema kuwa Kanisa Katoliki Matombo ni kanisa Mama katika jimbo la Morogoro Ukristo una historia ndefu Matombo kwa hiyo lisichezewe. Anashangaa kuona Wakristo wa Matombo wamebadilika na kuamini mambo ya kishirikina. Watu wanadanganywa na waganga kuwa wanatoa majini na vitu vingine. " Ni uongo, wanawadanganya, wanawalia pesa zenu nanyi mnabakia kuwa masikini. Nashangaa kuona mtu yuko tayari kuchangia fedha kumuita mganga wakati anashindwa kula vizuri, kuvaa vizuri na kuishi kwenye nyumba bora." Alilalamika Padri. Jakka. Aliongeza kwa kusema kuwa mtu utaachaje kuugua kama huogi, huli vizuri, unaendekeza pombe! Utawezaje kuwa na afya nzuri? Aliuliza.

Aliwasihi wakristu wa Matombo kuacha tabia ya kuendekeza ushirikina na kumrudia Mungu wetu. Alisisitiza kwa kusema kuwa tukio la leo litukumbushe kitu kimoja kuwa, kila mmoja wetu atakufa. Kwa njia ipi hiyo haifahamiki. Ni kweli kila mmoja wetu anaogopa kufa lakini lazima tufe. Kwa hiyo basi inatubidi tujitayarishe kwa kuishi maisha mema wakati wote.

No comments: