Tuesday, May 20, 2008

MWL. EPHREM EPHREM MBIKI HATUNAYE TENA

MWL. EPHREM EPHREM MBIKI HATUNAYE TENA

Tarehe 10 Mei, 2008 saa 8 mchana –Jumamosi, ukoo wa Wambiki ulimpoteza mtu muhimu sana katika ukoo huo naye si mwingine bali marehemu Mwl.Ephrem Ehprem Mbiki.

Kumbukumbu za mama yake mdogo Sista Maria Magdalena (Bibi Constancia Makeya) zanaeleza kuwa Mwl. Ephrem , kama alivyojulikana na wengi alizaliwa mwaka 1932 kijijini Nige, Matombo, Morogoro. Mwl. alikuwa ni mtoto wa tano kutoka familia ya watoto 9 wa Mzee Ephrem Kobelo Lugongo na Bibi Fransickka Makeya (wote marehemu).

Alipata Elimu yake ya Msingi – Matombo Middle School na hatimaye kujiunga katika Chuo cha Ualimu Kigurunyembe ambako alihitimu mwaka 1953. Mwaka 1954 alifunga ndoa na Bi. Fortunata Epimark wa Kigurunyembe Morogoro.

Katika uhai wake alifundisha katika shule zifuatazo: – Msata (Bagamoyo), Misegese –Mlali (Morogoro vijijini), Gozo-Matombo (Morogoro vijijini) na hatimaye shule ya msingi Matombo (Morogoro vijijini) kwa mkataba baada ya kustaafu.

Mwl. Ephrem alibahatika kupata jumla ya watoto 17 ambao hadi sasa walio hai ni 13 pamoja na wajukuu kadhaa.

Wanaomfahamu Mwl. Ephrem akiwemo mdogo wake Emili Wendelini “Bongwa” wameeleza kuwa marehemu atakumbukwa kwa kuwa alikuwa mshauri mzuri katika familia na aliweza kuikusanya na kuitambua popote ilipo, kiongozi wa dini hasa katika kusimamia Jumuiya Ndogo Ndogo, mtulivu na asiye na hasira, na alikuwa tayari kukosolewa na kushauriwa. Lakini pia alikuwa ni mcheshi kwa wakubwa na watoto.

Kama Mwalimu, alikuwa mwalimu mzuri ambaye aliweza kuboresha shule zote alizopitia. Kwa mfano alipohamishiwa shule ya msingi Gozo, wakati huo shule hiyo ilikuwa hadi darasa la nne tu, lakini yeye alifanikiwa kuipandisha chati hadi kufikia darasa la saba. Shuleni Msata, alimfundisha Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa darasa la kwanza.

MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MWL. EPHREM MBIKI

No comments: