Saturday, May 17, 2008

Moro-Matombo, barabara itengenezwe

Jumapili iliyopita nilisafiri kwenda kijijini kwetu Matombo-Morogoro kumzika baba yangu Mwl.Ephrem Ephrem Mbiki {Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.AMINA}.

Ni kilomita 65 kutoka Morogoro hadi Matombo (Nige-Kariakoo) lakini tulitumia masaa matatu na nusu. Tatizo barabara ni mbaya kwelikweli. Ubaya wa barabara unanzia Mkuyuni hasa sehemu za Mbehombeho na mlima wa Kibungo. Mashimo, mawe yaliyojitokeza barabarani na maji yanayotiririka na kuingia barabarani na kuharibu zaidi barabara. Pale Kibuno mlimani jiwe kuu liliporomoka na kuziba barabara. Ajabu katika kulipasua jiwe hilo bado teknolojia za zamani zinatumika kupasua kwa tindo!

Safari ya saa moja imetuchukua karibu masaa manne. Hii ni hatari sana. Ni hatari kwa maendeleo ya watu wa Matombo. Mamlaka husika haziwatendei haki wananchi wa Matombo. Wakulima wa Matombo ni wazalishaji wakubwa wa Matunda na mboga wanalisha kwa asilimia kubwa wakazi wa jiji la Dar Es Salaam, Morogoro, Dodoma hata Iringa. Yaonekana hakuna mipango madhubuti ya kuiweka barabara hiyo katika hali nzuri ya kuweza kupitika mwaka mzima. Matombo si maarufu kwa mazao ya kilimo tu. Madini ya aina mbalimbali yanapatikana Matombo. Kuna vivutio vya utalii katika mbuga ya Selous na milima ya Uluguru. Isitoshe mto wa Ruvu unaanzia kwenye milima ya Uluguru iliyoko Matombo. Tuamke na tuiboreshe barabara hiyo kwa manufaa ya watu wetu.

No comments: