Thursday, January 22, 2015

Tutangaze korosho kutoka Tanzania



Miaka ya 80 mpaka 90 zao la korosho lilikuwa hoi bin taabani. Wakulima wengi waliyaacha mashamba yao ya korosho na kuangalia shughuli nyingine zinazolipa. Jitihada zilizofanywa na serikali kupitia wadau mbalimbali zimenyanyua uzalishaji wa zao hilo. Korosho sasa bei yake imepanda si chini ya shilingi 1000 kwa kilo kwa korosho ambazo hazijabanguliwa. Sasa wajasiriamali wengi wamejitokeza na kuanza kuziandaa korosho na kuzifunga kwenye muonekano mzuri. Katika mkoa wa Mtwara, wilaya ya Tandahimba inaongoza kwa uzalishaji wa korosho na mabadiliko unayoona dhahiri kupitia maisha ya wananchi wa Tandahimba. Wanavijiji wana makazi bora, huduma za shule ni nzuri hata upatikanaji wa maji safi na salama zimeboreshwa kupitia ruzuku kutoka Halmashauri inayopatikana kutokana zaidi na kipato kutoka zao la korosho.Hebu angalia korosho zilizofungashwa vizuri kutoka IMANI. Korosho hizi zilikuwa kwenye maonyesho ya NaneNane 2014 mkoani Lindi viwanja vya Ngongo.Mimi ni mmoja ya watu wanaopenda kutafuna korosho hazinikinaishi. Korosho ni tamu. Hivi ni kwanini unaposafiri kwa usafiri wa anga, mashirika ya ndege hapa nchini hawatangazi korosho zetu za Tanzania kwa kuwapatia abiria watafune kama snacks? Ukipanda Air Botswana au Swazi utatafuna nyama zilizokaushwa mpaka meno yaume na kutambua kweli unaelekea nchi ya wafugaji!

No comments: