Thursday, June 26, 2008

Kibuku si pombe ya walalahoi

Jana mchana nilikutana na Bw Sicilima Kazonda - Meneja wa uzalishaji pombe aina ya Kibuku/Chibuku inayozalishwa na Kampuni ya DARBREW iliyopo Ubungo, Dar Es Salaam karibu kabisa na Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani. Ilikuwa ni safari ya kikazi kutaka kufahamu ni mali ghafi gani wanazotumia kutengeneza Kibuku na jinsi mkulima anavyoweza kufaidika kuwepo kwa DARBREW?

Kwanza nilifurahishwa na usafi wa hali ya juu niliouna kiwandani hapo. Meneja wa uzalishaji ofisi yake iko humohumo ndani ya sehemu za mitambo lakini kwa juu. Matanki pamoja na sakafu zilikuwa safi sana huwezi kuamini kama hapa ndipo panapotengenezwa kibuku ambayo wengi hufikiri kuwa ni pombe ya mlala hoi.

Kibuku hutengenezwa kwa mahindi meupe, mtama mweupe na mwekundu. Wataalamu kwa kutumia mali ghafi hizo huzalisha chibuku. Kwa sasa pombe hiyo hupatikana kwenye chupa ya plastiki (kibuku)pamoja na paketi za karatasi ngumu (chibuku) zote kwenye ujazo wa lita moja.

Nauliza swali. Je, hamchanganyi na maharage? Kwani nimepata kusikia watu wakisema kuwa moja ya mali ghafi ya chibuku ni maharage.

Si kweli, anakanusha Sicilima. Kwanza maharage ina protein nyingi kwahiyo haifai kutengeneza pombe kwani ikianza kuchachuka inatoa harufu mbaya. Watu wengi hudhani ni maharage kutokana na makapi ya mtama mwekundu.
Mtama mwekundu hutumika zaidi ili kupata rangi nyekundu.Anafafanua zaidi Sicilima.

Pombe hii ni bora kuliko pombe zinazotayarishwa kienyeji katika mazingira machafu na bila viwango ingawa hutumia malighafi zinazofanana. Bei yake ni poa (Tshs 400/= kwa lita). Labda ndiyo maana watu wanaiona ni ya walalahoi. Hata hivyo mtu yeyote anaweza kunywa chibuku. Hasa ukitilia maanani viwango (inapimwa kwenye maabara) na usafi katika utayarishaji wa chibuku.

Hiyo ndiyo chibuku. Sikuweza kuonja chibuku pale kiwandani lakini nadhani tatizo pombe hii haijatangazwa vya kutosha na walio wengi huifananisha na pombe nyingine za kienyeji.

Nchini Zambia Chibuku ni pombe maarufu sana na hutumiwa na watu wa aina mbalimbali wenye vipato na wasio na vipato vikubwa.

Wakati bia nyeupe inaendelea kupanda bei kwa kasi ya kutisha, wanywaji sasa wageukie Chibuku, si pombe ya walalahoi. Itumike hata kwenye sherehe za harusi bila kujificha!

Sicilima anamaliza kwa kusema kuwa mwaka huu wanampango wa kuongeza matumizi ya mtama kwa kutengeneza Chibuku kwani mahindi bei imeongezeka sana na ni adimu kupatikana kutokana na hali ya sasa ya upatikanaji wa mazao ya nafaka. Changamoto ipo kwenu wakulima na wadau wengine wa mtama. Lakini serikali pia iangalie swala la kodi ndiyo maana inauzwa aghali na kusababisha kupungua kwa mahitaji. Kama mahaitaji yanapungua makusanyo ya kodi nayo hupungua.

No comments: