Thursday, December 14, 2006

"UCHAWI WA SYRIA"

Mhandisi Phillip Mbuligwe amerudi leo leo kutoka Syria. Eeeh Mbuligwe, habari za Waarabu? Namuuliza tena kwa utani. "Acha wee Banzi, wale si Waarabu, wamepiga hatua kubwa kimaendeleo, siyo kama unavyofikiria wewe. Mimi nafikiri umezoea waarabu wa hapa "Bongo".

Ndiyo, Mbuligwe ni mhandisi. Mwezi Novemba, 2006 alikuwa kule Syria kwa mafunzo ya muda mfupi kuhusu umwagiliaji. Kwa maelezo yake, Phillip anasema kuwa, Syria hupata mvua mm 100 kwa mwaka, lakini wanajitosheleza kwa chakula. "Uchawi" mkubwa unaotumika kule ni umwagiliaji ndugu yangu anasema Phillip.

Umwagiliaji ni asilimia 100% katika kilimo. Siamini, naendelea kumdadisi. Sasa, mbona nasikia kule ardhi ni mchanga mtupu? Ni kweli, anaendelea kueleza Mbuligwe, Wasyria hufanya kila linalowezekana kupata maji. Huchimba visima virefu na pia hutumia maji ya mito inayokatiza katika ardhi yao. Serikali ilichofanya ni kutengeneza miundo mbinu ya umwagiliaji na kuendesha utafiti wa hali ya juu katika umwagiliaji.

Syria hutumia sana "Drip Irrigation" na "Sprinklers." Kwa njia hii wanatumia maji kufuatana na mahitaji ya mmea na maji hayapotei bure na kwakweli wakulima wanasema inalipa. Bila umwagiliaji, Syria isingeweza kuendesha kilimo.

Ndiyo, sasa wanalima mazao gani? Naendelea kumhoji. Aah Banzi kule kunastawi mazao mengi tu. Mbogamboga, ngano, matunda na hata mahindi. Lakini zao la chakula Syria ni ngano. Banzi, tikitimaji la Syria ni tamu utafikiri limewekwa asali anamalizia Mbuligwe.

Ndiyo, mtaalamu ndiyo huyo, amerudi toka Syria, amenieleza kuwa amejifunza mengi tena si kwa kuona tu au masomo ya nadharia, mafunzo yaliendeshwa kwa vitendo pia. Mbuligwe amerudi tumtumie kwenye utaalamu wa umwagiliaji.

Nilishawahi kusoma moja ya makala za Padri Privatus Karugendo (Kwa kweli huwa nasoma sana makala zake) anayeandikia gazeti la Rai. Katika makala hiyo, Karugendo anahoji, hivi kweli tumeshindwa kutumia vyanjo vyetu vya maji kwa umwagiliaji? Nafikiri vipaumbele vyetu vina walakini. Tujifunze basi kutoka Syria- 100 mm za mvua kwa mwaka, wanajitosheleza kwa chakula na "Tikitimaji ni tamu sana."

1 comment:

Ndesanjo Macha said...

Unaona wanafunzi tunawafundisha eti wakariri kuwa mto ruvu unapeleka maji yake bahari ya hindi na mto huu unapaleka maji yake ziwa hili, n.k. Inakuwa kama mito kupeleka maji baharini ni sifa badala ya sehemu ya maji hayo kutumika kwenye umwagiliaji.