Monday, March 8, 2010

Eti debe la viazi ni shilingi 2500/=


Blog ya Mjengwa leo imejaa picha za mazao yanayouzwa kwa bei ya kutupwa huko Makambako Iringa. Debe la viazi mviringo linauzwa kwa bei ya shilingi 2500/= . Maana yake ili aweze kununua bati moja itambidi auze madebe yasiyopungua sita. Madebe 180 ya viazi ndiyo yanayotosheleza kununua mabati 30 yanayotosho kuezeka nyumba ndogo.Katika hali hii si rahisi kukipenda kilimo.

Wednesday, March 3, 2010

Wachina na biashara ya magogo


Hivi karibuni sehemu ninayoishi mimi miembe kadhaa imeangushwa na kukatwa vipingili vidogo vidogo. Wilaya ya kilosa pia biashara ya magogo hasa ya miti ya mazao kama vile miembe na minazi imeshamiri. Na imebainika kuwa matajiri wa biashara hiyo ni Wachina. Wanavifanyia nini vigogo hivyo hatujui. Nani karuhusu biashara hiyo. Pia hatujui. Tusije kushangaa kukosa embe. Tusije kushangaa kukosa nazi. Haya yote ni ya kujitakia.

Pombe na UKIMWI

Hivi unywaji wa pombe unachangia kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa UKIMWI. Huko Iringa wanasemaje? "Msimu wa Ulanz\i huwa unauzwa bei rahisi ambayo hakuna inayemsinda ndo maana watu wengi hulewa hivyo kuwa rahisi kwao kufanya ngono bila kujiandaa kwani wanawake wengi wakishanunuliwa kinywaji hicho huwa wapesi kukubali," anasema Richard Mwenda. (Nukuu na picha kutoka gazeti la Mwananchi la 15/01/2010)

Tulikula mananasi


Wakulima wadogowadogo wanailisha Tanzania. Miezi mitatu iliyopita ilikuwa miezi ya mananasi. Jiji la Dar lilitapakaa kwa mananasi. Bahati mbaya mengi yalioza kwa kukosa teknolojia za kuhifadhi matunda au za kuongeza thamani.

Wakulima walio wengi wanalima kwa mazoea, wanalima kwa kubahatisha. Kilimo hapa Tanzania hakilipi sana. Miundo mbinu ni mibovu. Hakuna mitandao mizuri ya kuwawezesha wakulima kupata mikopo. Bila mikopo kilimo hakina faida. Huwezi kulima zaidi ya ekari mbili!

Ulanga kujenga nyumba za watumishi


Hivi karibuni wilaya ya Ulanga imetangaza mpango wa kujenga nyumba 14 za watumishi ambazo zitakaliwa na familia zipatazo 28. Kwa mujibu wa Mhandisi wa ujenzi wa wilaya hiyo, Hassan Matua mkakati wa ujenzi wa nyumba hizo umekuja baada ya kubaini kuwa watumishi wa sekta mbalimbali waliokuwa wakipangiwa kufanya kazi katika wilaya hiyo kukimbia kutokana na mazingira magumu pamoja na ukosefu wa nyumba. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na ni kivutio kwa wafanyakazi.

Miundo mbinu ya Jiji la Dar Es Salaam hoi!


Angalia pichani jinsi wananchi wanavyoteseka kutokana na miundombinu mibovu iliyoko Jijini Dar Es Salaam. Leo katika gazeti la Mwananchi nimeinyaka picha hii ikionyesha mkazi wa Rieta eneo la Makoka Mwisho jijini Dar Es Salaam akimvusha msichana wa shule katika daraja lililobomolewa kutokana na mafuriko ya mvua zilizonyesha hivi karibuni.

TAIFA STARS UBISHOO!


Wafadhili wa nguvu wamejitokeza kuihudumia Taifa Stars ( NMB, Serengeti Breweries). Kocha wa kimataifa Maximo wanaye. Wapenzi wapo wanaishangilia kwa nguvu inapocheza. Mshiko mwanangu wa uhakika.Hebu angalia pichani wachaezaji wa Taifa Stars wakifanya mazoezi wakiwa na pamba za Serengeti wanapendeza eti! Tatizo inapokwa kwenye mashindano upuuzi mtupu. Tatizo ni ubishoo na kujifanya wamefika. Hebu mwangalie huyu mchezaji wa mbele tayari ameshafuga nywele kama Valderama!

Nguvu ya CCJ inatoka wapi?


Hivi nguvu ya Chama kipya cha CCJ (Chama cha Jamii) inatoka wapi?

  • Vigogo kutoka CCM?
  • CCM inashabiiana sana na CCJ?
  • Rangi zake ukiondoa kijani unabakia na njano kama CCM tu?
  • Au ushabiki tu wa vyama vya upinzani
Wanasiasa na vyama vya upinzani nipeni JIBU

Friday, February 26, 2010

Tunaita kudandia


Haya ndiyo watoto wetu wanayoweza.
Kijana huyu ni umri wa wanafunzi wa shule za msingi. Sasa tujiulize anadandia bus ili iweje? Hana sare za shule pengine tungesema kuwa anataka kuwahi kwenda shule. Hapa ni Dar hiyo ndiyo Taswira ya Taifa. Picha kutoka Gazeti la Mwananchi la Tarehe 26/2/10

Ushindi ni mazoezi


Asikudanganye mtu, ushindi ni mazoezi tu. Angalia jinsi mlinda mlango wa Twiga Queens (Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake)- Zena Juma anavyojifua kwenye mazoezi. Hii inampa stamina, uzoefu pamoja na mbinu. Hivyo vyote vikikamilika ushindi ni dhahiri. MUNGU IBARIKI TWIGA QUEENS

Mjibu Kipanya basi


Kama wewe mjuzi wa kujibu maswali mjibu kipanya tukate mzizi wa fitina wa rushwa.

Kuna nini UWT



UWT kuna fukuto kali. Vijembe na mambo kadha wa kadha. Wengine hatufahamu chochote. Lakini jinsi nilivyomsikia Makamu wa Mwenyekiti wa chama hicho Bi Asha Makame kwa kipitia TBC 1 jana jioni na leo hii kusoma kwenye gazeti la Mwananchi lenye kichwa cha Habari "Mwilima ajiandaa kujibu mapigo UWT." Gazeti hilo lilimnukuu Mwilima akisema "Mmhh! Napata utata kulijibu hilo, lakini nisema tu kwamba kwa mujibu wa katiba ya UWT, kikao cha Kamati ya Utendaji ndicho kinachoweza kuniondoa," alisema Mwilima.

Tuesday, February 23, 2010

Anauza mikate!


Leo asubuhi nimeinyaka picha hii kutoka kwenye blog ya ndugu yangu Mjengwa. Picha hii imepigwa Zanzibar. Mfanyabiashara huyu raha mustarehe anauza mikate kwenye tenga huku akiitangaza waziwazi bila kufunikwa. Usalama wa afya za walaji je. Hata huku Tanzania Bara tabia hii ya wafanyabiashara kutojali usalama wa afya za walaji ni tatizo sugu. Utaona samaki wa kukaanga wanauzwa barabarani bila kuhifadhiwa, korosho zimewekwa kwenye mafungu na kuguswaguswa na wanunuzi. Hii kwa kweli si tabia nzuri. Wafanyabiashara wajifunze utaratibu mzuri wa kuuza bidhaa zao hasa vyakula.

Monday, February 22, 2010

Kumbe Ulaya nako barabara mbovu kama bongo!


Unaulizwa, kama msichana huyu alikupita wakati ukimuomba lift. Ukimkuta kwenye hali hii utamsaidia?

Hee mizigo mitano kwenye pikipiki!


Mzee anaendesha, huku akipakia binti, nyumba ndogo na mama pamoja na tenga. Wakipata ajali ni kazi ya Mungu? Pikipiki hii haikutengenezwa kwa madhumuni hayo.

Hii ndiyo JWTZ


Kwa mazoezi haya na mengine ambayo hayawezi kuonyeshwa ovyo ovyo. Jeshi letu si mchezo. Mtu akija kicha kichwa ataumizwa vibaya sana oh! Safi sana JWTZ!

Anayesema hakuna chochote kwenye sekta ya KILIMO mwongo


Angalia kwenye picha wataalamu wakiwa kwenye viatu vya kazi (boots) mwangalie Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifurahia shamba zuri la mahindi kwa ajili ya kuzalisha mbegu linalomilikiwa na JKT Mlale wilaya ya Mbinga.

Kisu kimenolewa acha kabisa mchezo


Ndiyo, baada ya kukaa muda mrefu kwa maumivu, Ulimboka Mwakingwe 'Uli' amerudi na makali mapya dimbani kwenye kikosi cha Wekundu wa Msimbazi (SSC). Kasi imeongezeka na shabaha ya goli kama kawa! Kuna nini tena mbona kazi kwisha. Ubingwa ni dhahiri mwaka huu. Pichani Uli katika kasi yake akimtoka Stephen Mwasika wa Moro United katika mchezo wa ligi kuu uwanja wa UHURU hapo jana (21/02/2009). Simba ilishinda kwa magoli 4-1. Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

Friday, February 19, 2010

Kumbe chocolate kwa kiswahili ni kashata!


Hii nimeinyaka leo kutoka blog ya uncle Michuzi. Kuna chocolate inayotenngezwa kwa jina la Tanzania. Nasikia inapendwa sana huko majuu. Sasa uncle yeye ameiita ni kashata. Sikujua kama chocalate ndiyo kashata. Tuanze kutumia sasa mtoto akitaka chocolate dukani basi tunasema nipe kashata mbili za maziwa (milk chocolate)!

Vyakula dawa vinavyorefusha maisha



Leo katika pekuapekua yangu nimekuta kilichotayarishwa na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kinachoelezea vyakula dawa vinavyorefusha maisha kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Vyakula hivyo ni Viungo (husaidia kutuliza au kutibu matatizo ya afya kama kutapika, kuharisha, mafua, kichefuchefu na kujaa gesi tumboni. Mboga na Matunda ni chanzo cha vitamini na madini muhimu mwilini husaidi kuongeza damu, uzito na vitamini A . Mimea kama ubuyu wenye vitamini C hutuliza mafua na kuongeza hamu ya kula, choya (rozela) husaidia pia kuongeza damu. Shubiri (alovera) husaidia kutibu magonjwa mbalimbali yakiwemo malaria na kisukari. Kipeperushi hicho kinapatiokana kupitia barua pepe: psk@kilimo.go.tz