Thursday, April 3, 2014

Usafi wa makaburi Parokiani Matombo



Usafi wa makaburi ni muhimu. Wakristu Wakatoliki wa Parokia zote huwa na utaratabu wa kufagilia makaburi angalau mara mbili kwa mwaka kabla ya Sikukuu ya Pasaka na tunapokaribia sikukuu ya watakatifu wote. Sehemu hizi wamezikwa Babu na Bibi zetu, Baba na Mama zetu, Shangazi na wajomba zetu, Kaka na Dada zetu, Watoto wetu marafiki na ndugu wengine. Ni ajabu kuona wakristu tunategea kufanya usafi wa sehemu za makaburi ingawa utaratibu upo kwa kila Parokia. Kufagilia makaburi hakuhitaji uwezo wa kifedha, la hasha, kinachohitajika ni utashi na nia ya kujituma kwa kutumia nguvu alizotupa Mungu wetu.

Nilipotembelea kijiji changu hivi karibuni na kupata bahati ya kusali na kuhiji kwenye makaburi yetu sikufurahishwa na hali niliyoiona. Upande mmoja makaburi yamesafishwa na kunapendeza (Picha ya kati). Sehemu nyingine (Picha ya chini) kuna nyasi nyingi kiasi cha kushindwa kutambua alipozikwa ndugu yako au mzazi wako. Naipongeza Jumuiya (picha ya Juu) iliyojipanga na kufanya usafi. Ndugu zangu wa Matombo IMANI yetu na moyo wa kujitolea vimepotelea wapi? Hivi kweli tumefikia mahali kuwa hata kusafisha makaburi lazima tutoe fedha? Nawasihi kuwa wakati tunajiandaa kwa PASAKA usafi wa makaburi upewe kipaumbele.

No comments: