Leo asubuhi nimekuwa nikipitia makala moja iliyoandikwa kwenye Gazeti la Raia Mwema la tarehe 14 Oktoba (Toleo Maalum). Makala hiyo imeandikwa na Jaji Mark Bomani. ambayo ni hotuba iliyotolewa na Jaji Mark Bomani wakati akitangaza nia yake ya kuwania urais wa Tanzania kupitia CCM mwaka 1995. Katika hotuba yake , Bomani alisema kiini cha matatizo yetu ya maendeleo ni UMASIKINI. Katika miaka ya sitini miaka michache baada ya uhuru tulipiga hatua kubwa katika kuzalisha mali. Kwa mfano uzalishaji wa zao la mkonge ulifikia zaidi ya tani 220,000 kwa mwaka-tukishika nafasi ya kwanza duniani; zao la korosho nalo lilikuwa zaidi ya tani 150,000 kwa mwaka; Pamba ilifikia marobota zaidi ya 400,000 kwa mwaka. Kahawa na Chai yalikuwa ni mazao maarufu yakituletea fedha nyingi za kigeni. Nchi yetu ilizalisha mazao ya chakula kwa wingi na hatukulazimika kuagiza chakula toka nchi za nje: mahindi, mchele,sukari, ngano na mengine. Vipi bonde la Kilombero lisiweze kututosheleza kwa zao la mpunga? Vipi maeneo ya Kilombero, Kagera na Mtibwa yasizalishe sukari ya kututosheleza?
Zambia ilikuwa haizalishi sukari hata tani moja mpaka ilipoanzisha kilimo cha miwa katika bonde la Nakambala mwaka 1968, yaani baada ya Uhuru. Baada ya miaka 10 Zambia ilikuwa inajitosheleza kwa mahitaji yake ya sukari na kuuza nci za nje?
Malawi ambayo ni kama robo tu ya Tanzania inazalisha sukari na mpunga kutosheleza mahitaji yake na kuuza nje. Leo Swaziland inazalisha sukari nyingi kuliko sisi-inakuwaje? Sioni kwa nini Tanzania ishindwe kujitosheleza kwa zao hili wakati zao la sukari limeanza kulimwa hapa nchini hata kabla ya uhuru!
Nchi yetu ina matunda ya kila namna ambayo tungejua namna ya kuyahifadhi, kama vile wanavyofanya Afrika ya Kusini, tungeyala mwaka mzima na hata kuuza nchi za nje.
Sera ya hifadhi ya chakula (food security) bado nayo haijapata msukumo wa uhakika. Lazima sera hii ipewe kipaumbele na juhudi za kuitekeleza kwa haraka. Kusema kweli wageni wengi pamoja na mabalozi wa nchi za nje waliopo hapa nchini ambao nimekutana nao hawaelewi inawezekana vipi Tanzania ikawa ni nchi maskini wakati ina mali asili nyingi hivi pamoja na ardhi yenye rutuba, maziwa na mito mingi!
Namibia ni nchi yenye madini na samaki kwa wingi. Vinginevyo sehemu yake kubwa ni jangwa. Ina ulingo wa bahari wa kilometa 1000. Inavua samaki hadi kufikia tani 700,000 kwa mwaka, wakati fulani walifikia tani milioni moja! Sisi hapa Tanzania licha ya maziwa makubwa, mito chungunzima na ulingo wa bahari wa kilometa 800, jumla ya samaki tunaovua kwa mwaka ni chini ya tani 500,000!
Uzalishaji wa mazao muhimu umeshuka. Kwa mfano zao la mkonge limeshuka toka tani 220,000 hadi tani 40,000 kwa mwaka! Zao la korosho ndiyo kwanza hivi karibuni limefikia tani 40,000. Zao la Pamba linapanda na kushuka kati ya marobota 450,000 na 350,000, yaani baada ya miaka 34 ya uhuru tumeshindwa kuzalisha pamba zaidi.
Zao la mkonge lazima lifufuliwe, tena kwa haraka iwezekanavyo, ili taifa lijipatie pato kubwa kutokana na matumizi ya zao hilo. Wale mnaoweza kukumbuka wakati wa enzi za ukoloni, zao la Mkonge liliupatia Mkoa wa Tanga umaarufu mkubwa kiasi kwamba Gavana wa Tanaganyika, kila mwaka alikuwa anakwenda Tanga kutangaza mipango ya kiuchumi ya Serikali ya Tanganyika.
Lazima kuwarejeshea mkoa wa Tanga umaarufu huo. Kila jitahada itafanywa ili Tanzania irudie umaarufu wake wa kuwa nambari wani katika uzalishaji wa zao la katani.
Vyama vya ushirika (hasa vya Pamba na Kahawa) kuanzia Mwanza mpaka Mbinga vilikuwa ni mfano wa kujivunia duniani. Vyama hivi ndivyo vilivyoshika hatamu ya kuhamasisha na kusukuma mbele kilimo nchini. Viliwahudumia wananchi katika kupata mbegu bora, kupata pembejeo kwa bei nafuu, kununua mazao ya wananchi, na kuwauzia wananchi vijijini bidhaa mbalimbali. Lakini baada ya vyama hivi kufutwa hapo mwaka 1976 na baadaye kurejeshwa mwaka 1982 , havijaweza kurudisha afya zao za awali.
Ni dhahiri mapinduzi katika sekta ya kilimo yatategemea sana uimarishaji wa vyama vya ushirika nchini kote.Hili ni jukumu muhimu la kufanyiwa kazi.
Viwanda mbalimbali muhimu, hasa vile vinavyotumia malighafi ya humuhumu nchini, kama vile viwanda vya kutengenezea nguo, viwanda vya kusindika nyama, viwanda vya kubangua korosho, viwanda vya kulainisha ngozi (tanneries) navyo tulivijenga tukiwa na matumaini makubwa katika uzalishaji mali na utoaji wa ajira.
Leo hii hi ni viwanda vichache tu ambavyo bado vinafanya kazi! Inakubalika vipi nchi yenye kulima Pamba kwa wingi iachie viwanda vya kutengeneza nguo vife au visimame na badala yake taifa litegemee nguo za kutoka nchi ambazo wala hazilimi Pamba! Na hizi fedha za kigeni zinazotumika kuagizia hizi nguo bila ya nchi kuuza bidhaa za kutosha nchi za nje zinatoka wapi?
Inakubalika vupi nchi yenye ng'ombe zaidi ya milioni 15 isiwe na hata kiwanda kimoja cha kusindika nyama? Tanganyika Packers imesimama miaka mingi; kiwanda cha kusindika Nyama cha Shinyanga hakijaanza hata kufanya kazi, baada ya kujengwa kwa gharama ya mamilioni ya shilingi!
Inakubalika vipi nchi iliyokuwa maarufu kwa zao la korosho ijenge viwanda 12 vya kubangulia Korosho kwenye miaka ya 70 na halafu vyote isipokuwa kimoja tu ndicho kiwe kinafanya kazi?
Inakubalika vipi kwa nchi iliyokuwa inashika nafasi ya kwanza duniani katika kuzalisha zao la mkonge na ambayo ilijenga kiwanda cha kusokota nyuzi za Katani kikubwa kuliko vyote duniani na leo kiwanda hicho kiachwe kife hivi hivi tu!
Huu ni udhaifu dhahiri kabisa katika uongozi wetu wa uchumi. Na halafu tuambiwe kwamba eti dawa ni ubinafsishaji! Lazima tuwe na sera mpya za kufufua na kuendeleza viwanda vyetu nchini na kutoa msukumo katika kulinda viwanda vyetu.
Hivi sasa mjadala umejitokeza kuhusu sera ya ubinafsishaji. Mjadala huu umepamba moto baada ya hotuba ya Baba wa Taifa ya Mei Mosi huko Mbeya, hotuba ambayo iligusia msimamo wake kuhusu sera ya ubinafsishaji. Wapo wanaohoji kwamba mashirika ya umma yamekuwa ni mzigo mkubwa kwa wananchi na kwamba itikadi ya uchumi inayozaa matunda ni ile inayolenga umilikaji wa mali kupitia watu binafsi. Wanahoji kwamba ubinafsishaji wa viwanda ni mkakati madhubuti wa kuimarisha viwanda na uchumi wa taifa kwa ujumla na kwamba fikra za Mwalimu zinatokana na kushikilia sera za soko la nguvu badala ya nguvu za soko.
Napenda kusema kwamba Chama Cha Mapinduzi kimekwisha toa sera na mwalekeo kwa miaka 90. Sera hiyo inasema na nina nukuu: "Lengo la Ujamaa na Kujitegemea katika miaka ya tisini litakuwa kuhakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu, mmoja mmoja, kwa kupitia vyama vyao huru vya ushirika wa aina mbalimbali, kwa kupitia makampuni ya wananchi na ya ubia ambao maelfu ya wananchi watanunua hisa, na kwa kupitia umilikaji wa dola kwa mashirika yale yatakayoendelea kuwa mikononi mwake.
Kwa mtazamo huu CCM sehemu kubwa ya uchumi wa nchi inakusudiwa imilikwe na wananchi wenyewe ili kuinua hali ya maisha yao na kutosheleza mahitaji yao ya msingi. Dola, pamoja na kuendelea kumiliki sekta muhimu na ya msingi ya uchumi na huduma, itaendelea kushika nafasi za muhimili wa uchumi wa taifa." Mwisho wa kunukuu.
Sera ya CCM haizungumzii ubinafshaji kama itikadi. Sera hii inazingatia kwamba dola itaendelea kuwa na mashirika msingi mikononi mwake. Si hivyo tu, Sera ya CCM inalenga umilikaji wa wananchi wenyewe katika kuendesha uchumi. Hii haina maana kwamba CCM haikubali wawekezaji toka nchi za nje, la hasha. Chama cha Mapinduzi kinapendelea kukuwa kwa wawekezaji wa kitaifa (national investors) ambao ndiyo watakaoweza kushirikiana na wawekezaji toka nchi za nje.
Nchi zinazoendelea haraka haraka kama vile Taiwan, Korea ya Kusini, Singapore, Malaysia, Indonesia na hata India, ni nchi ambazo zimejenga msingi madhubuti wa uwekezaji wa kitaifa na jazitegemei sana wawekezaji toka nchi za nje katika kukuza uchumi wao. Nchi hizi zilikuwa na sekta kubwa tu za dola lakini ubinafshaji wao ulifanikiwa kwa sababu zilikuwa tayari zimejenga wawekezaji wa kitaifa. Lakini Tanzania yetu ya leo ina wawekezaji wa kitaifa wachache mno waliozungukwa na maskini wengi! Wananchi wengi, wakulima na wafanyakazi, ambao ndiyo tunaamini wangeweza kununua hisa katika makampuni yanayobinafsishwa hali zao ndiyo kwanza zimedidimia.
Na hata kama tungeafiki mfumo potofu wa kuwa na matajiri wachache katika umma maskini, hao matajiri, hasa wenye viwanda, hali zao pia hivi sasa ni taabani.
Kwa hiyo sera yetu ya ubinafsishaji imekosa tafakuri ya kina ambayo inabidi ijibu swali kwa nini sekta nzima ya viwanda nchini, iwe chini ya miliki ya watu binafsi au dola, imezorota na kufifia. Je, tutabinafsisha sekta binafsi pia?
No comments:
Post a Comment