Tuesday, November 12, 2013

Mtei-Hawezi kusahau tukio la kujiuzulu ugavana

Mzee Edwin Mtei
"Siwezi kusahau kipindi ambacho nilijiuzulu ugavana kwani tulitofautiana sana na Mwalimu (Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere) hadi nikaamua kuuza nyumba yangu Dar Es Salaam na kuhamia Arusha, na hapa nimekuwa mkulima hadi leo. Unajua Mwalimu alikuwa mtu asiyependa demokrasia hata kidogo, alikuwa mtu ambaye haambiliki, yeye alipenda kile alichokisema tu kitekelezwe.

Mwaka 1977 Mwalimu Nyerere walitofautiana na Mzee Kenyata na alifunga mpaka wa Tanzania na Kenya, wakati huo Milton Obote (Rais wa Uganda enzi hizo) alikuwa ameporwa madaraka na Idd Amin na ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikavurugika. Mimi nikiwa ni Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo niliamua kurudi nyumbani.

Niliporudi  nikapewa nafasi ya kuwa Waziri wa kwanza wa Fedha, wakati huo tukiwa katika vita ya Uganda na mimi ndiye nilikuwa nikisimamia masuala ya uchumi na fedha wakati wote wa vita. Vita ilipoisha nchi yetu iliingia katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, hatukuwa na fedha kabisa.

Ndipo nikamua kumshauri Mwalimu, kwamba tukope fedha katika Benki ya Dunia ili kutatua suala hili. Baada ya kushauriana na watu wa Benki ya Dunia nilimwambia Mwalimu pia tupunguze bajeti ya matumizi yetu, nilimshauri vitu vingi kwa kweli.

Unajua, Mwalimu alinijibu kwamba mimi nimeshawishiwa na watu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ndipo nikamuua kujiuzulu. Huwezi kuamini na siku najiuzulu, Mwalimu alitoa hotuba ya kuridhia kujiuzulu kwangu na kusema kwamba  'kamwe hawezi kuruhusu serikali yake iongozwe kutoka Washington.'

Hakika nilishtushwa na hotuba yake baada ya mimi kujiuzulu ukizingatia ya kwamba mimi nilikuwa nimelitumikia taifa langu kwa uadilifu mkubwa, ndipo nikaamua kuwa mkulima hadi leo. Niliuza nyumba yangu Dar Es Salaam na kununua shamba kubwa hapa Tengeru mkoani Arusha.

Mwalimu alipenda watu wa kumwambia 'ndiyo mzee' na bahati mbaya mimi sikuwa mtu wa namna hiyo. Kila alichokisema alitaka kifuatwe na hata umma unajua kwamba mimi nilithubutu kumwambia Mwalimu 'hapana.'

Nukuu kutoka gazeti la Mwananchi la Oktoba 14, 2013 katika mahojiano yaliyofanywa na mwandishi Moses Mashalla na  Mzee Edwin Mtei aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

No comments: