Tuesday, November 12, 2013

Butiku anasema nini kuhusu Nyerere?

Kuna wakati napata bahati kusoma makala mbalimbali  kutoka magazetini. Ni vizuri wasomaji wangu nanyi mkasoma yanayoandikwa.

Mwandishi Exuper Kachenje wa gazeti la Mwananchi  katika mahojiano yake na Mzee Joseph Butiku ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na ambaye aliwahi kuwa Katibu Myeka wa Mwalimu Nyerere alimuuliza Mzee Joseph Butiku kuwa 'Binafsi amechota nini kutoka kwake (Mwl. Julius Kambarage Nyerere). Butiku alijibu "Nimechota uadilifu, ukweli, heshima kwa watu wote, kujali watu na kujitahidi kuwa mtu kwa watu wengine. Mwalimu alikuwa 'role model' (mtu wa mfano) wangu. Kitu ambacho sikuweza kuchota kwake, ni imani yake katika utu na usawa kwa wote, niliona imani hiyo na iliendana na imani yake katika kumcha Mungu na jitahada zake kuhudumia watu kadri ya imani yake ya Kikristo.

Mwalimu alikuwa mtu mwenye kuona mbali, alipenda umoja, amani kubwa na ndogo, mwadilifu, mtu maalumu aliyetumia muda wake wote kutumikia watu wengine. Tunaweza kusema, sisi tunajitahidi kufuata yake, lakini hatujamfikia bado tuna upungufu." Alipoulizwa swali , "Mwalimu aliwahi kusema CCM siyo baba yake, wala mama yake. Unafikiri bado angeendelea kuwapo ndani ya CCM au angewaambia nini Watanzania? Butiku alijibu. "Sidhani kama angerudisha kadi kwa CCM, siwezi kumsemea maana hayupo, lakini nadhani angeendelea kuwa mzee anayeishauri CCM, kuhakikisha kwamba haiendelei kupotoka, ikiacha misingi yake na angeendelea kuvishauri vyama vya upinzani ili vifanye kazi zao kwa ufanisi zaidi. Kabla ya kufariki kwake, Mwalimu alisema hajaona chama cha upinzani kinachoweza kutawala Tanzania, ndiyo maana alibaki CCM. Mimi naishauri CCM izingatie misingi na sera zake."

No comments: