Friday, November 29, 2013

Gari lililobeba mwili wa marehemu Emmanuel Kishongo

Gari lililobeba mwili wa marehemu Emma Kishongo likielekea makaburini Mzumbe -Changarawe

R.I.P. Emmanuel Kishongo

Jeneza lililobeba mwili wa mdogo wangu Emmanuel Kishongo likiwa ndani ya kaburi. R.I.P. Emma.

Thursday, November 14, 2013

Hivi hiyo shikamoo inatolewa na nani?


Pengine tunajiandaa kwa kombe la Dunia 2021!

Kama kweli vile!

Rooney anaposhangilia ushindi

Manchester United ya Uingereza si klabu ninayoishabikia licha ya kuvaa jezi rangi nyekundu! Mimi huko timu yangu ni Liverpool (pengine ni kasumba tu) na duniani timu yangu ninayoishabikia ni Barcelona (si kwa sababu ya Messi lakini  ni soka yao yenye mvuto). Naipenda pia Beyern  Munich ya Ujerumani kwa jitahada zao wawapo uwanjani. Lakini pia naipa saluti Manchester kwa kujituma  kwao, wamekuwa mwiba kwa Arsenal kwa muda mrefu sasa.

Asante Airtel kwa kukumbuka wanafunzi

Meneja Masoko wa Airtel  wa Kanda ya Kusini na Mkoa wa Morogoro akikabidhi  vitabu vya sayansi kwa mwanafunzi wa kidato cha Tatu kutoka shule ya Sekondari ya Chalinze

Wanasimba tukishangilia mpaka mwisho wa game

Baada ya kutangulia goli 3-0  kipindi cha kwanza - Yanga walifikiri mchezo umekwisha walisahau kuwa zimebaki dakika 45. Ndipo walipostukia magoli matatu yakirudi yoteee. Na hapa tikishangilia kwa kwenda mbele. Chezea mnyama weye!

Mr. "Chakulia" wa Yanga

Kama hamumfahamu , huyu ndiye Mr. Chakulia wa Dar Young Africans yenye makao yake makuu  Jangwani, jijini Dar Es Salaam, Tanzania. Siku yangu ilipofungwa 5-0  Mr. "Chakulia" alilia sana

Mkapa picha ya miaka 75 na Maaskofu

Mhe. Benjamin William Mkapa  (mwenye suti katikati), Rais wa awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na mkewe (kushoto kwake) pamoja na Cardinal Polycarp Pengo  (mwenye joho la dhahabu) na maaskofu wengine katika picha ya pamoja baada ya kuadhimisha ibada ya misa takatifu ya SHUKRANI ya kutimiza miaka 75 ya kuzaliwa  kwake tarehe 12/11/2013. Ibada imefanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Imakulata, Upanga, jijini Dar Es Salaam 9picha kwa hisani ya gazeti la Dailnews 14/11/2013)

Zawadi ya Mwakilishi wa Papa kwa Mkapa

Balozi wa VATICAN nchini Tanzania Archbishop Francusco Montecillo Paddila  alitoa ujumbe maalumu kwa  Mhe. Benjamin Mkapa wakati wa Ibada ya Shukrani ya kutimiza miaka 75 ya kuzaliwa kwa Mkapa ambaye alikuwa Rais wa awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibada hiyo ilifanyika tarehe 12/11/2013 ndani ya Kanisa Katoliki la Mt.Imaculata lililopo Upanga, Jijini Dar Es Salaam. (Picha kwa hisani ya gazeti la Dailynews 14/11/2013)

Mkapa miaka 75 ya kuzaliwa-NENO LA SHUKRANI

Rais wa awamu ya Tatu - Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Mhe. Benjamin Mkapa akitoa NENO LA SHUKRANI  kumshukuru MUNGU kutimiza miaka 75 ya kuzaliwa kwake tarehe 12/11/2013. Misa ya shukrani ilifanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Imakulata, Upanga, jijini Dar Es Salaam. (Picha kwa hisani ya gazeti la Dailynews 14/11/2013).

Miaka 75 ya Mhe. Benjamin Mkapa Ibada kanisani

Ndugu na jamaa na wageni waalikwa walishiriki Ibada ya misa ya Shukrani ya kutimiza miaka 75 ya kuzaliwa iliyoombwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Benjamin William Mkapa. Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa Katoliki  la Upanga -Mt.Imakulata tarehe 12/11/2013. Si wengi wanaokumbuka kutoa SHUKRANI kwa jambo jema kama hili. HONGERA ! (Picha zote kwa hisani ya gazeti la Dailynews  14/11/2013)

BENJAMIN MKAPA MIAKA 75

Tarehe 12/11/2013 aliyekuwa Rais wa awamu ya Tatu Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa  alitimiza miaka 75 ya kuzaliwa kwake. Pichani akiongoza maandamano na mkewe kulekea kanisani-Upanga kwa misa ya shukrani. HONGERA! (Picha kwa hisani ya gazeti la Daily News 14/11/2013)

Wednesday, November 13, 2013

Bado hatujapambana na umaskini-Bomani

Leo asubuhi nimekuwa nikipitia makala moja iliyoandikwa kwenye Gazeti la Raia Mwema la tarehe 14 Oktoba (Toleo Maalum). Makala hiyo imeandikwa na Jaji Mark Bomani. ambayo ni hotuba iliyotolewa na Jaji Mark Bomani wakati akitangaza nia yake ya kuwania urais wa Tanzania kupitia CCM mwaka 1995. Katika hotuba yake , Bomani alisema kiini cha matatizo yetu  ya maendeleo ni UMASIKINI. Katika miaka ya sitini miaka michache baada ya uhuru tulipiga hatua kubwa katika kuzalisha mali. Kwa mfano uzalishaji wa zao la mkonge ulifikia zaidi ya tani 220,000 kwa mwaka-tukishika nafasi ya kwanza duniani; zao la korosho nalo lilikuwa zaidi ya tani 150,000 kwa mwaka; Pamba ilifikia marobota zaidi ya 400,000 kwa mwaka. Kahawa na Chai yalikuwa ni mazao maarufu yakituletea fedha nyingi za kigeni. Nchi yetu ilizalisha mazao ya chakula kwa wingi na hatukulazimika kuagiza chakula toka nchi za nje: mahindi, mchele,sukari, ngano na mengine. Vipi bonde la Kilombero lisiweze kututosheleza kwa zao la mpunga? Vipi maeneo ya Kilombero, Kagera na Mtibwa yasizalishe sukari ya kututosheleza?

Zambia ilikuwa haizalishi sukari hata tani moja mpaka ilipoanzisha kilimo cha miwa katika bonde la Nakambala mwaka 1968, yaani baada ya Uhuru. Baada ya miaka 10 Zambia ilikuwa inajitosheleza kwa mahitaji yake ya sukari na kuuza nci za nje?

Malawi ambayo ni kama robo tu ya Tanzania inazalisha sukari na mpunga kutosheleza mahitaji yake na kuuza nje. Leo Swaziland inazalisha sukari nyingi kuliko sisi-inakuwaje? Sioni kwa nini Tanzania ishindwe kujitosheleza kwa zao hili wakati zao la sukari limeanza kulimwa hapa nchini hata kabla ya uhuru!

Nchi yetu ina matunda ya kila namna ambayo tungejua namna ya kuyahifadhi, kama vile wanavyofanya Afrika ya Kusini, tungeyala mwaka mzima na hata kuuza nchi za nje.

Sera ya hifadhi ya chakula (food security) bado nayo haijapata msukumo wa uhakika. Lazima sera hii ipewe kipaumbele na juhudi za kuitekeleza kwa haraka. Kusema kweli wageni wengi pamoja na mabalozi wa nchi za nje waliopo hapa nchini ambao nimekutana nao hawaelewi inawezekana vipi Tanzania ikawa ni nchi maskini wakati ina mali asili nyingi hivi pamoja na ardhi yenye rutuba, maziwa na mito mingi!

Namibia ni nchi yenye madini na samaki kwa wingi. Vinginevyo sehemu yake kubwa ni jangwa. Ina ulingo wa bahari wa kilometa 1000. Inavua samaki hadi kufikia tani 700,000 kwa mwaka, wakati fulani walifikia tani milioni moja! Sisi hapa Tanzania licha ya maziwa makubwa, mito chungunzima na ulingo wa bahari wa kilometa 800, jumla ya samaki tunaovua kwa mwaka ni chini ya tani 500,000!

Uzalishaji wa mazao muhimu umeshuka. Kwa mfano zao la mkonge limeshuka toka tani 220,000 hadi tani 40,000 kwa mwaka! Zao la korosho ndiyo kwanza hivi karibuni limefikia tani 40,000. Zao la Pamba linapanda na kushuka kati ya marobota 450,000 na 350,000, yaani baada ya miaka 34 ya uhuru tumeshindwa kuzalisha pamba zaidi.

Zao la mkonge lazima lifufuliwe, tena kwa haraka iwezekanavyo, ili taifa lijipatie pato kubwa kutokana na matumizi ya zao hilo. Wale mnaoweza kukumbuka wakati wa enzi za ukoloni, zao la Mkonge liliupatia Mkoa wa Tanga umaarufu mkubwa kiasi kwamba Gavana wa Tanaganyika, kila mwaka alikuwa anakwenda Tanga kutangaza mipango ya kiuchumi ya Serikali ya Tanganyika.

Lazima kuwarejeshea mkoa wa Tanga umaarufu huo. Kila jitahada itafanywa ili Tanzania irudie umaarufu wake wa kuwa nambari wani katika uzalishaji wa zao la katani.

Vyama vya ushirika (hasa  vya Pamba na Kahawa) kuanzia Mwanza mpaka  Mbinga vilikuwa ni mfano wa kujivunia duniani. Vyama hivi ndivyo vilivyoshika hatamu ya kuhamasisha na kusukuma mbele kilimo nchini. Viliwahudumia wananchi katika kupata mbegu bora, kupata pembejeo kwa bei nafuu, kununua mazao ya wananchi, na kuwauzia wananchi vijijini bidhaa mbalimbali. Lakini baada ya vyama hivi kufutwa hapo mwaka 1976 na baadaye kurejeshwa mwaka 1982 , havijaweza kurudisha afya zao za awali.

Ni dhahiri mapinduzi katika sekta ya kilimo yatategemea sana uimarishaji wa vyama vya ushirika nchini kote.Hili ni jukumu muhimu la kufanyiwa kazi.

Viwanda mbalimbali muhimu, hasa vile vinavyotumia malighafi ya humuhumu nchini, kama vile viwanda vya kutengenezea nguo, viwanda vya kusindika nyama, viwanda vya kubangua korosho, viwanda vya kulainisha ngozi (tanneries) navyo tulivijenga tukiwa na matumaini makubwa katika uzalishaji mali na utoaji wa ajira.

Leo hii hi ni viwanda vichache tu ambavyo bado vinafanya kazi! Inakubalika vipi nchi yenye kulima Pamba kwa wingi iachie viwanda vya kutengeneza nguo vife au visimame na badala yake taifa litegemee nguo za kutoka nchi ambazo wala hazilimi Pamba! Na hizi fedha za kigeni zinazotumika kuagizia hizi nguo bila ya nchi kuuza bidhaa za kutosha nchi za nje zinatoka wapi?

Inakubalika vupi nchi yenye ng'ombe zaidi ya milioni 15 isiwe na hata kiwanda kimoja cha kusindika nyama? Tanganyika Packers imesimama miaka mingi; kiwanda cha kusindika Nyama cha Shinyanga hakijaanza hata kufanya kazi, baada ya kujengwa kwa gharama ya mamilioni ya shilingi!

Inakubalika vipi nchi iliyokuwa maarufu kwa zao la korosho ijenge viwanda 12 vya kubangulia Korosho kwenye miaka ya 70 na halafu vyote isipokuwa kimoja tu ndicho kiwe kinafanya kazi?

Inakubalika vipi kwa nchi iliyokuwa inashika nafasi ya kwanza duniani katika kuzalisha zao la mkonge na ambayo ilijenga kiwanda cha kusokota nyuzi za Katani kikubwa kuliko vyote duniani na leo kiwanda hicho kiachwe kife hivi hivi tu!

Huu ni udhaifu dhahiri kabisa katika uongozi wetu wa uchumi. Na halafu tuambiwe kwamba eti dawa ni ubinafsishaji! Lazima tuwe na sera mpya za kufufua na kuendeleza viwanda vyetu nchini na kutoa msukumo katika kulinda viwanda vyetu.

Hivi sasa mjadala umejitokeza kuhusu sera ya ubinafsishaji. Mjadala huu umepamba moto baada ya hotuba ya Baba wa Taifa ya Mei Mosi huko Mbeya, hotuba ambayo iligusia msimamo wake kuhusu sera  ya ubinafsishaji. Wapo wanaohoji kwamba mashirika ya umma yamekuwa ni mzigo  mkubwa kwa wananchi na kwamba itikadi ya uchumi inayozaa matunda ni ile inayolenga umilikaji wa mali kupitia watu binafsi. Wanahoji kwamba ubinafsishaji wa viwanda ni mkakati madhubuti wa kuimarisha viwanda na uchumi wa taifa kwa ujumla na kwamba fikra za Mwalimu zinatokana na kushikilia sera za soko la nguvu badala ya nguvu za soko.

Napenda kusema kwamba Chama Cha Mapinduzi kimekwisha toa sera na mwalekeo kwa miaka 90. Sera hiyo inasema na nina nukuu: "Lengo la Ujamaa na Kujitegemea katika miaka ya tisini litakuwa kuhakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu, mmoja mmoja, kwa kupitia vyama vyao huru vya ushirika wa aina mbalimbali, kwa kupitia makampuni ya wananchi na ya ubia ambao maelfu ya wananchi watanunua hisa, na kwa kupitia umilikaji wa dola kwa mashirika yale yatakayoendelea kuwa mikononi mwake.

Kwa mtazamo huu CCM sehemu kubwa ya uchumi wa nchi inakusudiwa imilikwe na wananchi wenyewe ili kuinua hali ya maisha yao na kutosheleza mahitaji yao ya msingi. Dola, pamoja na kuendelea kumiliki sekta muhimu na ya msingi ya uchumi na huduma, itaendelea kushika nafasi za muhimili wa uchumi wa taifa." Mwisho wa kunukuu.

Sera ya CCM haizungumzii ubinafshaji kama itikadi. Sera hii inazingatia kwamba dola itaendelea kuwa na mashirika msingi mikononi mwake. Si hivyo tu, Sera ya CCM inalenga umilikaji wa wananchi wenyewe katika kuendesha uchumi. Hii haina maana kwamba CCM haikubali wawekezaji toka nchi za nje, la hasha. Chama cha Mapinduzi kinapendelea kukuwa kwa wawekezaji wa kitaifa (national investors) ambao ndiyo watakaoweza kushirikiana na wawekezaji toka nchi za nje.

Nchi zinazoendelea haraka haraka kama vile Taiwan, Korea ya Kusini, Singapore, Malaysia, Indonesia na hata India, ni nchi ambazo zimejenga msingi madhubuti wa uwekezaji wa kitaifa na jazitegemei sana wawekezaji toka nchi za nje katika kukuza uchumi wao. Nchi hizi zilikuwa na sekta kubwa tu za dola lakini ubinafshaji wao ulifanikiwa kwa sababu zilikuwa tayari zimejenga wawekezaji wa kitaifa. Lakini Tanzania yetu ya leo ina wawekezaji wa kitaifa wachache mno waliozungukwa na maskini wengi! Wananchi wengi, wakulima na wafanyakazi, ambao ndiyo tunaamini wangeweza kununua hisa katika makampuni yanayobinafsishwa hali zao ndiyo kwanza zimedidimia.

Na hata kama tungeafiki mfumo potofu wa kuwa na matajiri wachache katika umma maskini, hao matajiri, hasa wenye viwanda, hali zao pia hivi sasa ni taabani.

Kwa hiyo sera yetu ya ubinafsishaji imekosa tafakuri ya kina ambayo inabidi ijibu swali kwa nini sekta nzima ya viwanda nchini, iwe chini ya miliki ya watu binafsi au dola, imezorota na kufifia. Je, tutabinafsisha sekta binafsi pia?

Sababu tatu za Mwl.Nyerere kung'atuka


Balozi Charles Sanga aliyefanya kazi na Mwalimu kama Msaidizi wake maalumu katika miaka yake saba ya mwisho hapa duniani,katika mahojiano yake na gazeti la Rai Mwema,  ameweka wazi sababu tautu kuuu zilizomfanya Mwl. Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa) kung'atuka.
  1. Yeye ni binadamu na hivyo ipo siku atakufa tu na kuachia madaraka. Kama  ana hofu kwamba hakuna Mtanzania mwingine anayeweza kushika urais, je akifa itakuaje?
  2. Mwalimu alisema kama yeye asingeachia madaraka, hakuna kiongozi mwingine wa Tanzania ambaye angekubali kuachia madaraka. Hivyo alitaka kutengeneza mfumo au utaratibu wa kupokezana vijiti. "Kwa maelezo yake mwenyewe Mwalimu alisema kama tutaweza kupokezana madaraka kwa muda wa miaka 30 hadi 40 mfululizo, huo utakuwa utaratibu wa kudumu na hakuna atakayeupindua.
  3. Tatu, Mwalimu alisema alitaka kuangalia mwenyewe na kusaidia pale inapowezekana kwenye masuala ya kitaifa. Kuhakikisha Katiba inafuatwa, Awe nje lakini afuatilie kile kinachoendelea na kuona kwamba mpokezano huu wa madaraka unaendelea.

Tuesday, November 12, 2013

Matokeo ya Darasa la saba kwa Wilaya ya Morogoro Vijijini ni kilio

Shule ya msingi Lanzi
Banzi wa Moro ni mzaliwa wa Morogoro vijijini, tarafa ya Matombo. Jana nilipata nafasi ya kutathmini matokeo ya Darasa la saba kwa mwaka 2013 kwa wilaya ya Morogoro vijijini kwa shule chache ninazozifahamu kama vile Matombo, Konde, Kitungwa, Gozo, Kibungo,Kibangile, Tununguo, Nyachiro,Lanzi,Kungwe. Wastani wa ufaulu kwa shule hizi ni D. Nina maswali mengi yasiyo na majibu. Je, shule hazina walimu? Mazingira si mazuri, hakuna ushirikiana kati walimu na wazazi? Wangapi wameiona hali hii. Wangapi wanakerwa na matokeo haya? Kwetu sisi Moro matokeo haya si mazuri. Shule iliyojitahidi ni ya  3044 kitaifa nayo ni Kibangile. Shule za siku nyingi kama vile Matombo ni ya 10705 kitaifa? Hivi Matombo ina shida gani? Wazawa kutoka Morogoro tuyafanyie kazi matokeo haya  na tuje na mapendekezo. Kwa mfano picha ya hapo juu inaonyesha darasa mojawapo ya shule ya msingi Lanzi. Sijui kama kuna mabadiliko (Picha kutoka mitandaoni)

Mama Salma Kikwete na vazi la Kimasai

  Mimi nawapenda Wamasai kwa kutunza mila na desturi zao. Ukiongea na Wamasai vizuri wanazo sababu za msingi  kuhusu mavazi yao, chakula chao na mfiugo yao.

Mwl. Nyerere akipiga ngoma


Nimekuwa nikiiona picha hii ya Baba wa Taifa akipiga ngoma na huku mtoto akimwangalia kwa makini. Kumbe mtoto huyo ni mwanae Madaraka Nyerere. Kwa kweli ni picha nzuri ya ukumbusho. Hivi sasa Madaraka ni mtu mzima kabisa!   (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi 14/10/2013)

Nyerere alimsaidia Raila Odinga kusoma nje

Raila Odinga akisalimiana na Mhe.Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
"Harakati za kupigania uhuru ni pamoja na kuwasaidia wengine wanaowekewa vikwazo na wanaowatawala." Raila Odinga, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya ambaye sasa ni kiongozi mkuu wa Muungano wa Cord alipata Pasipoti ya Tanzania iliyotolewa na Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere iliyomuwezesha kusafiri kwenda Ujerumani kwa masomo. Taarifa hii ni kutoka gazeti la Mwananchi la tarehe 14/10/2013.

Nyerere na Wasaidizi wake

Enzi hizo, Baba wa Taifa Mwl. Julius Kamabarage Nyerere akiongea na wasaidizi wake. Ninaowakumbuka pichani mwenye suti nyeusi ni Hayati Abdulrahaman Babu, Kushoto ni Joseph Sinde Warioba na wa pili kutoka kulia mwenye miwani ni Benjamin William Mkapa. (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi Oktoba 14, 2013)

Butiku anasema nini kuhusu Nyerere?

Kuna wakati napata bahati kusoma makala mbalimbali  kutoka magazetini. Ni vizuri wasomaji wangu nanyi mkasoma yanayoandikwa.

Mwandishi Exuper Kachenje wa gazeti la Mwananchi  katika mahojiano yake na Mzee Joseph Butiku ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na ambaye aliwahi kuwa Katibu Myeka wa Mwalimu Nyerere alimuuliza Mzee Joseph Butiku kuwa 'Binafsi amechota nini kutoka kwake (Mwl. Julius Kambarage Nyerere). Butiku alijibu "Nimechota uadilifu, ukweli, heshima kwa watu wote, kujali watu na kujitahidi kuwa mtu kwa watu wengine. Mwalimu alikuwa 'role model' (mtu wa mfano) wangu. Kitu ambacho sikuweza kuchota kwake, ni imani yake katika utu na usawa kwa wote, niliona imani hiyo na iliendana na imani yake katika kumcha Mungu na jitahada zake kuhudumia watu kadri ya imani yake ya Kikristo.

Mwalimu alikuwa mtu mwenye kuona mbali, alipenda umoja, amani kubwa na ndogo, mwadilifu, mtu maalumu aliyetumia muda wake wote kutumikia watu wengine. Tunaweza kusema, sisi tunajitahidi kufuata yake, lakini hatujamfikia bado tuna upungufu." Alipoulizwa swali , "Mwalimu aliwahi kusema CCM siyo baba yake, wala mama yake. Unafikiri bado angeendelea kuwapo ndani ya CCM au angewaambia nini Watanzania? Butiku alijibu. "Sidhani kama angerudisha kadi kwa CCM, siwezi kumsemea maana hayupo, lakini nadhani angeendelea kuwa mzee anayeishauri CCM, kuhakikisha kwamba haiendelei kupotoka, ikiacha misingi yake na angeendelea kuvishauri vyama vya upinzani ili vifanye kazi zao kwa ufanisi zaidi. Kabla ya kufariki kwake, Mwalimu alisema hajaona chama cha upinzani kinachoweza kutawala Tanzania, ndiyo maana alibaki CCM. Mimi naishauri CCM izingatie misingi na sera zake."

Mtei-Hawezi kusahau tukio la kujiuzulu ugavana

Mzee Edwin Mtei
"Siwezi kusahau kipindi ambacho nilijiuzulu ugavana kwani tulitofautiana sana na Mwalimu (Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere) hadi nikaamua kuuza nyumba yangu Dar Es Salaam na kuhamia Arusha, na hapa nimekuwa mkulima hadi leo. Unajua Mwalimu alikuwa mtu asiyependa demokrasia hata kidogo, alikuwa mtu ambaye haambiliki, yeye alipenda kile alichokisema tu kitekelezwe.

Mwaka 1977 Mwalimu Nyerere walitofautiana na Mzee Kenyata na alifunga mpaka wa Tanzania na Kenya, wakati huo Milton Obote (Rais wa Uganda enzi hizo) alikuwa ameporwa madaraka na Idd Amin na ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikavurugika. Mimi nikiwa ni Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo niliamua kurudi nyumbani.

Niliporudi  nikapewa nafasi ya kuwa Waziri wa kwanza wa Fedha, wakati huo tukiwa katika vita ya Uganda na mimi ndiye nilikuwa nikisimamia masuala ya uchumi na fedha wakati wote wa vita. Vita ilipoisha nchi yetu iliingia katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, hatukuwa na fedha kabisa.

Ndipo nikamua kumshauri Mwalimu, kwamba tukope fedha katika Benki ya Dunia ili kutatua suala hili. Baada ya kushauriana na watu wa Benki ya Dunia nilimwambia Mwalimu pia tupunguze bajeti ya matumizi yetu, nilimshauri vitu vingi kwa kweli.

Unajua, Mwalimu alinijibu kwamba mimi nimeshawishiwa na watu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ndipo nikamuua kujiuzulu. Huwezi kuamini na siku najiuzulu, Mwalimu alitoa hotuba ya kuridhia kujiuzulu kwangu na kusema kwamba  'kamwe hawezi kuruhusu serikali yake iongozwe kutoka Washington.'

Hakika nilishtushwa na hotuba yake baada ya mimi kujiuzulu ukizingatia ya kwamba mimi nilikuwa nimelitumikia taifa langu kwa uadilifu mkubwa, ndipo nikaamua kuwa mkulima hadi leo. Niliuza nyumba yangu Dar Es Salaam na kununua shamba kubwa hapa Tengeru mkoani Arusha.

Mwalimu alipenda watu wa kumwambia 'ndiyo mzee' na bahati mbaya mimi sikuwa mtu wa namna hiyo. Kila alichokisema alitaka kifuatwe na hata umma unajua kwamba mimi nilithubutu kumwambia Mwalimu 'hapana.'

Nukuu kutoka gazeti la Mwananchi la Oktoba 14, 2013 katika mahojiano yaliyofanywa na mwandishi Moses Mashalla na  Mzee Edwin Mtei aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Friday, November 8, 2013

Hivi ni vyetu

Hizi ni bidhaa zetu. Watanzania tununue na kuwashauri wabunifu hawa jinsi ya kuongeza ubora wa bidhaa zao. Wajasiriamali nao  waangalie bei za bidhaa zao. Tunakimbia kununua bidhaa zao kwa sababu zilizo nyingi bei haiendani na ubora wa bidhaa hizo. (picha kwa hisani ya gazeti la mwananchi)

Wadau wa Korosho kikaoni Dar

Hivi karibuni wadau wa Korosho walikutana jijini Dar kujadili mstakabali wa kuongeza thamani kwa zao la korosho (Picha na Dr. Louis Kasuga, ARI-Naliendele)

Darasa linapogeuzwa bweni

Huku ni kuwatesa watoto na kushusha hadhi ya elimu hapa nchini. Inawezakanaje darasa kuwa bweni? (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi)

Simba walipoliandama lango la Ashanti

Simba ikiwa katika pilika la kufnga langoni mwa goli la Ashanti . Simba ilishinda 4-2 (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi)

P-square kutua Dar

Hawa ndiyo P-Square wanaotarajia kutua jijini Dar Es Salaam mwezi huu (Novemba -2013) kwa show la nguvu litakalofanyika katika viwanja vya Leaders

Ndani ya Kanisa - Parokia ya Chang'ombe

Hivi ndivyo linavyonekana kanisa la Chang'ombe kwa ndani (Picha kwa hisani ya Dr. Louis Kasuga)

Kanisa Katoliki Parokia ya Chang'ombe

Jengo la Kanisa Katoliki -Parokia ya Chang'ombe, Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Miaka tisa iliyopita  ndiyo ilikuwa parokia yangu.

Huyu ndiye Betty Missokia wa Haki-Elimu

Bi.Elizabeth Missokia (Kulia) CEO wa Haki -Elimu akiongea na waandashi wa habari hivi karibuni (picha kwa hisani ya gazati la mwananchi).

Hakika 100% Moro

Morogoro mji kasoro bahari! Maarufu kwa soka, muziki,kilimo na utalii!

Thursday, November 7, 2013

Mtambo mpya bandarini Dar Es Salaam

Mtambo mpya wa kupakua na kupakia mizigo umetua bandarini Dar.  (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi)

Mwanamama mchoma mihogo Arusha

Mwanamama  Victoria Emmanuel akiwa amembeba mwanae akichoma mihogo na ndizi jijini Arusha.
Hakuna shughuli ya mwanaume tu kila mtu anaweza kufanya shughuli yoyote ukiwa na nia. Tukijishughulisha riziki inapatikana!

Wadada wamekabidhiwa bendera

Wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake U-20 (The Tanzanite) wamekabidhiwa bendera na kuondoka jana kuelekea nchini Msumbiji. Tunawatakia ushindi 9picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi)

Kilimanjaro beer mali ya Tanzania

Fikiria kijua cha saa sita. Halafu unapewa kituliza kiu cha Kilmanjaro beer iliyo baridi. Sijui utajisikiaje! Hii ni mali ya Tanzania. Beer safi - Premium Lager - sasa imetoa chupa mpya ya ml 375 kwa bei ya Tshs 1600. Hongera Tanzania Breweries. Banzi wa Moro ndo kinywaji chake. Angalau vibia  2 kwa siku!

Korosho utazipenda tu!

Kama hujawahi kutafuna korosho basi picha hii ni kishawishi tosha za kuanza kula korosho halafu utaniambia. Mikoa yote ya pwani nchini Tanzania inazalisha korosho lakini mikoa ya kusini (Mtwara na Lindi ) ni maarufu zaidi. Na huku ndiko kiliko kituo cha Utafiti Naliendele  ambako wako watafiti waliobobea na utafiti wa korosho. Sasa wamekuwa gumzo  barani gumzo jinsi wanavyolipandisha chati zao la korosho.

Korosho kutoka kituo cha Utafiti Naliendele


Korosho safi tamu zinavutia kutoka kituo cha Utafiti Naliendele, Mtwara.Watafiti wa zao la korosho walipo kwenye kituo cha Utafiti  Naliendele mkoani Mtwara  wamefika mbali zaidi, si tu wanatafiti mbegu bora, kinga ya magonjwa na wadudu, rutuba ya udongo. Sasa wamefikia mlaji hiyo ndiyo moja ya bidhaa zao kutoka korosho wanazotafiti. Hii ni mali ya Watanzania. Watanzania tuchangamkie kilimo cha korosho fedha iingie mifukoni mwetu.

Tuesday, November 5, 2013

Ha mboga ya maboga

Mboga ya maboga imeshachumwa kutoka shambani. Iko kwenye maandalizi ya kupikwa katika kibanda cha mamalishe kijijini  Mvumi, Kilosa, Morogoro.

Satelitte Dish kijijini Mvumi

    Mambo mazuri  vijijini. Ukizungumzia  Messi wote wameshamuona kupitia Luninga. Haya ndiyo maendeleo kwa mazingira haya walimu, mabwanashamba, waganga, wahandisi na wataalamu wengine watapenda kuishi vijijini.

NGO ya kuhamasisha usafi

    Vijijini  kuna Asasi zisizo za Kiserikali nyingi (NGO) kama hiyo inayohamsisha watu kunawa mikono       sabuni kabla ya kula

Kibanda cha kujiremba- Mvumi

Hiki ni kibanda cha kutengeneza nywele kwa akina baba kijijini Mvumi, Kilosa, Morogoro

Nyumba bora mazingira safi kijijini Mvumi

    Nyumba bora mazingira safi na ya kupendeza kijijini Mvumi,Kilosa-Morogoro

Huduma ya mawasiliano inapatikana Mvumi

Kijijini Mvumi, Kilosa, Morogo-huduma ya mawasiliano kwa mitandao ya Vodacom na Tigo  inapatikana.Pia unaweza kutoa  na kutuma pesa kama inavyoonekana pichani. Maendeleo vijijini!

Vifaa vya mamalishe wa Mvumi

Hivi ndivyo vifaa vya mamalishe  wa Mvumi. Kuna mchele, mafuta, ndoo za maji, jiko la mkaa na simu ya mawasiliano sakafuni!

Duka la nyama (Butcher) kijijini Mvumi

Maisha mazuri popote. Hata kijijini Mvumi, wilayani Kilosa kuna duka la nyama zuri.

Ndani ya Bus safarini Mvumi kwa mazishi

Tukiwa na mwili wa marehemu Lawrence Mbunda  safarini kwa mazishi kuelekea Mvumi, Kilosa Morogoro kwa mazishi.

Diwani John Waziri na matango

Diwani John Waziri wa Halmashauri ya mjini wa Morogoro akichagua matango kijijini Mvumi, Kilosa, Morogoro alipokwenda kwa mazishi ya marehemu Lawrence Mbunda, tarehe 3/11/2013

Kibanda cha mamalishe Mvumi

Kibanda cha mamalishe kinachoendelea kujengwa kijijini Mvumi, Kilosa, Morogoro.

Mapumziko ndani ya kibanda cha mamalishe

Dada zangu waliokwenda msibani Mvumi walijipumzisha ndani ya kibanda cha Mamalishe.