Monday, July 21, 2008

Hata Kisemvule wanafahamu Shamba Darasa


Jana Jumapili tarehe 20/06/2008 ilikuwa siku muhimu sana katika kumbukumbu ya maisha yangu. Jana, kwa mara ya kwanza niliweza kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Kijiji ninachoishi, kijiji cha Kisemvule kilichopo wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani. Kilomita 27 kutoka mahali ninapofanyia kazi jijini Dar Es Salaam.


Agenda kuu muhimu katika kikao hicho zilikuwa ni kuwakilisha utekelezaji wa bajeti ya kijiji kwa mwaka 2007/08 na mapendekezo ya Bajeti ya Kijiji kwa mwaka 2008/09. Nilichofurahishwa ni kuona jinsi gani mawasilisho hayo yalivyowasilishwa vizuri tena kwa kitaalamu na jinsi wanakijiji walivyozijadili taarifa hizo kwa ufasaha na kupatiwa ufumbuzi.


Nilifurahi zaidi nilipoona nguvu ya wanakijiji pale walipoweka kipaumbele cha kununua madawawati ya shule ya msingi Kisemvule kwanza baada ya kupata taarifa kuwa shule ina madawati 34 tu. Walisema kuwa uendelezaji wa ujenzi wa ofisi ya kijiji usubiri kwanza.


Jingine lililojitokeza ni pale mwanakijiji mmoja alipouliza nini maana ya shamba darasa baada ya kusikia kwenye bajeti ya mwaka 2008/09 sekta ya kilimo kuwa moja ya shughuli zitakazofanywa na kijiji ni pamoja na kuwa na shamba darasa. Mwanakijiji huyu alipata maelezo ya ufasaha kutoka kwa mwanakijiji mwenzake kuhusu shamba darasa. Pamoja na kwamba mimi nafahamu vizuri kuhusu shamba darasa, maelezo yaliyotolewa na mwanakijiji yule yalikuwa sahihi ndiyo maana nasema hata Kisemvule wanafahamu Shamba Darasa. Kazi kwenu wataalamu wa Kilimo pelekeni teknolojia.

No comments: