Thursday, July 3, 2008

Mwandishi wa Habari Henry M.Stanley

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2008 nilitembelea kanda ya Magharibi hasa mkoa wa Tabora kwa shughuli ya kukagua na kutathmini kazi za utafiti kwenye kanda hiyo. Nikiwa huko nilipata fursa ya kutembelea moja ya makumbusho ya Taifa yaliyopo Tabora barabara ya kwenda Sikonge. Pale pana mambo mengi ya ukumbusho. Kwanza kuna jumba kubwa la tembe (sasa limekarabatiwa). Jumba hilo lilikuwa la mwarabu mmoja aliyejishughulisha sana na biashara ya utumwa. Baadaye lilinuliwa na wajerumani na kufanyiwa marekebisho. Ndani kuna nakala za machapisho ya gazeti la NewYork Herald -1872 zilizoandikwa na Henry M.Stanley mwandishi wa habari mahiri aliyetumwa kumtafuta Dr.David Livingstone aliyefia Afrika lakini maiti yake ilizikwa kwao kwa kubebwa na waafirika Susi na Chuma ambao walikuwa ni wasaidizi wa Livingstone wakati wa safari zake. Ndani ya jumba hilo kuna minyororo ya utumwa, kuna msalaba wa mzungu John Shaw aliyejipiga risasi na kuzikwa hapohapo Tabora, kuna kigoda alichokalia Stanley kuna barua alizoandika Livingstone kwenda kwa rafiki yake Benjamin Pyne n.k.

Utakapofika kwenye kituo hicho kuna bango la chuma lenye maandishi haya:- " David Livingstone after he had met H.M.Stanley at Ujiji on Nov.10.1871 he left this spot on August 25.1872 to undertake what was to be his last journey in Africa."

No comments: