Wednesday, June 27, 2012

WASIFU WA DR.GREGORY P.C.MLUGE

Picha ya ukumbusho wa Dr. Gregory P.C.Mluge (katikati)enzi za uhai wake akiwa na mkewe Restituta (wa kwanza kushoto) wakitambulishwa na mpwa wao Inno Banzi wakati wa sherehe za komunio ya kwanza ya watoto wake nyumbani kwao Kisemvule-Pwani
Dr. Gregory Paul Constance Mluge alizaliwa tarehe 12 Machi 1937,wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani ambako baba yake Mwalimu Paul Lugonzo alikuwa anafundisha. Dr. Gregory Mluge alizaliwa katika familia ya Bw.Paul Lugonzo na Bibi Annastazia Hugo Mlachuma. Alikuwa mtoto wa pili kwenye familia ya watoto saba wakiwemo wanawake watano na wanaume wawili. Kati ya hao Sr. Philomena, Janeth, Rosemary na Frederick wametangulia mbele ya haki. Waliobaki ni Beatrice na Dolores. Marehemu Dr.Mluge alianza masomo yake ya msingi huko Bagamoyo na baadaye familia ilirudi Matombo, Kiswira ambako marehemu Paul Lugonzo aliendelea kufundisha katika Shule ya MsingiMatombo. Dr. Mluge alisoma shule za msingi Matombo na Bigwa. Aliendelea na masomo ya sekondari shule ya wavulana Tabora na baadaye shule ya sekondari maarufu hapa nchini ya Pugu. Dr. Mluge alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere , Kampala Uganda kutoka mwaka 1960 hadi 1965 ambako alipata shahada yake ya kwanza ya udaktari. Alianza kazi ya udaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam. Baada ya mwaka mmoja alihamishiwa hospitali ya mkoa Tabora. Baada ya muda aliteuliwa kuwa daktari mkuu wa wilaya ya Nzega mkoa wa Tabora mwaka 1967. Hapo Nzega alikutana na afisa wa wauguzi ambaye alimpenda kwa jina Restituta Emmanuel Assenga wa Rombo Mashati mkoani Kilimanjaro ambaye alimrushia ndoana ya huba naye Restituta akanasa. Ukawa mwanzo wa uchumba na hatimaye kufunga ndoa. Dr. Mluge alipewa ‘scholarship’ ya kwenda Uingereza kuendelea na masomo ya udaktari bingwa mwaka 1969. Huko Uingereza alisomea diploma ya ‘Tropical Public Health’, katika chuo cha London School of Tropical Medicine na kupata stashahada. Mwaka 1971 huko Uingereza alipokea tena stashahada ya ‘Tropical medicine and Hygiene’. Mwaka 1972 hadi 1973 alisoma na kuhitimu shahada ya uzamili ya ‘Occupational medicine’ kutoka chuo kikuu cha London. Mwaka huo huo pia alisomea na kupokea shahada ya ‘Industrial health’ na mwaka 1973 hadi 1975 alipata shahada ya tatu ya medicine na cheo cha MRCP kutoka chuo kikuu cha London. Alifanya kazi katika hospitali bingwa mbalimbali nchini Uingereza kuanzia mwaka 1975 hadi 1980. Alipendwa sana na madaktari wenzake na wagonjwa wake wote. Mtoto wake pekee Janeth Mluge Schoemaeiker alizaliwa mwaka 1978. Mwaka 1980 Dr. Mluge aliajiriwa kama Proffessor wa udaktari na afya ya Jamii na mwalimu wa madaktari wadogo katika Chuo Kikuu cha Jeddah nchini Saudi Arabia. Mwaka 1989 alirudi Tanzania kufanya kazi zake mwenyewe, lakini mwaka huo huo aliombwa na serikali ya Saudi Arabia kurudi tena na kuendelea na kazi ya Proffessor huko. Alifanya kazi huko pamoja na mke wake Restituta ambaye alikuwa Mkurugenzi huko Saudi Arabia. Familia ya Dr. Gregory Mluge iliamua kurudi Tanzania mwaka 2006. Dr. Gregory Mluge alikuwa ni mtu aliyependa sana watu wote, mkarimu sana, aliyewasaidia watu wengi katika nyanja zote za maisha ikiwemo kitabibu, kielimu, kiushauri na mengine mengi ambayo nina imani itahitaji muda mwingi kuyataja yote. Dr. Mluge alikuwa ni mtu mwenye msimamo wa kweli. Alikuwa mkweli, mvumilivu sana, daktari mzuri na mpole sana. Na kwa hayo yote tunasema AHSANTE SANA. Dr. Mluge alikuwa mpenzi wa kilimo,ujenzi,na magari lakini ‘hobby’ yake kubwa ilikuwa muziki, na katika hilo alikuwa bingwa wa kupiga kinanda. Marehemu Dr. Mluge ameacha mjane, mtoto mmoja ,wajukuu wawili na dada wawili. RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA! NA MWANGA WA MILELE UMUANGAZIE, APUMZIKE KWA AMANI….AMINA.

No comments: