Friday, June 29, 2012
Zambia fedha nyingi kunyakua ubingwa Afrika
Waziri wa Michezo wa Zambia, Chisimba Kambwili amesema Serikali ya Zambia ilitumia kiasi cha Kwacha 1.2 bilioni (Dola 235,865) kwa ajili ya kuiandaa timu ya taifa ya soka ya Zambia "Chipolopolo" iliyotwaa ubingwa wa Afrika 2012.
Kambwili alisema baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika wachezaji walipewa posho mbalimbali ambazo zilifikia Kwacha 11.5 bilioni (Dola 2,260,380).
Waziri huyo alisema hayo katika Bunge la Zambia wakati alipokuwa akijibu swali aliloulizwa ni kiasi gani cha fedha kilitumika kwa ajili ya kuiandaa Chipolopolo iliyotwaa ubingwa wa Afrika 2012 na kiasi gani wachezaji hao walipewa baada ya kushinda ubingwa huo wa Afrika.
Hata hivyo waziri huyo aliiponda Serikali ya zamani ya Zambia iliyokuwa ikiongozwa na chama cha siasa cha MMD.Alisema Serikali iliyopita ilikuwa ikigombana mara kwa mara na Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ). Waziri Kambwili alisema Serikali iliyopita ya Zambia chini ya Rais Rupiah Banda ilimuajiri kocha wa timu ya taifa Dario Bonetti bila kuomba ushauri kutoka FAZ hali iliyoonyesha na kusababisha soka la Zambia kushuka.
"Kama watu wa Zambia wasingekiweka chama cha PF madarakani na kuunda serikali, basi kombe la Mataifa ya Afrika lisingekuja Zambia. Ninao ushahidi wa ninachokisema, watu wengi Zambia wanajua, dunia inajua kwamba Serikali ya MMD ilimleta kocha Bonetti bila kuishauri FAZ," alisema Kambwili.
"Soka ilikuwa imepoteza mwelekeo, chama cha PF kilipoingia madarakani na mimi kuingia wizara ya michezo hatukukuta bajeti ya kuiandaa timu ya taifa kwa sababu ya uongozi wa Serikali iliyopita ilikuwa haifanyi kazi vizuri na FAZ,viongozi walikuwa wakifanya hivyo ili FAZ, ionekane haiwezi kazi yao," alisema Kambwili.
Alisema chama cha PF chini ya Rais Michael Sata kiliposhinda uchaguzi na kuunda Serikali ya Zambia kiliandaa bajeti ya kuisaidia timu ya taifa na kuiweka timu kambini nchini Afrika Kusini.
"Serikali ya MMD ilikuwa haitaki timu iweke kambi Afrika Kusini na ilikuwa inataka timu iweke kambi Ndola, lakini PF tulipoingia madarakani tuliwapa FAZ fedha na timu ikaweka kambi Afrika Kusini kwa sababu ya kulingana hali ya hewa na nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon zilipokuwa zikifanyika fainali za kombe la Mataifa ya Afrika 2012, matokeo yake Zambia ikatwaa ubingwa wa Afrika.
"Hivyo napenda kuwaambia viongozi wa chama cha MMD kwamba hawakufanya chochote katika ubingwa wa Afrika wa Zambia, ila ubingwa huo ulitokana na mipango mizuri ya chama cha PF," Alisema.(Habari na picha kwa hisani ya gazeiti la Mwananchi 29/6/2012). JE KUNA UKWELI WA MAELEZO HAYA? TAFAKARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment