Friday, August 1, 2008

"TIGO" PEKEE WAMEWAONA WAKULIMA?


Sikukuuu ya wakulima "NANE NANE" ndiyo hiyo imeingia. Lakini kwa mujibu wa gazeti la "This Day." Kampuni ya simu "TIGO" ndiyo inayoonekana kudhamini maonyesho hayo tena kwa shilingi milioni 10 tu!

Kampuni nyingine ziko wapi? Kuna kampuni ambayo hainufaiki na Kilimo? Mbona kimya? Hata huo ufadhili wa shilingi milioni 10 kutoka TIGO ni mdogo sana. Hivi kuna wakulima wangapi wanaotumia mtandao wa TIGO? Hata kwetu Matombo, Morogoro mtandao unaotamba ni "TIGO" mnara wake umewekwa mlimani kileleni hivyo kuwafunika kabisa Celtel mtandao wa kwanza Matombo.

Huo ndio mtazamo wa watanzania wengi kwenye kilimo, hatukipi stahili yake kwenye mipango yetu licha ya mchango mkubwa unaotoa kwenye uchumi wa Taifa na maisha ya wananchi wetu.

Nashangaa " Serengeti" wamedhamini mpira wa miguu kwa mamilioni ya fedha huku wakisahau kuwa bia wanazotengeneza, malighafi kubwa ni mazao ya kilimo (ngano na shayiri).

Tunakula nyama za aina mbalimbali (kuku, ng'ombe, mbuzi, kondoo, bata) kutokana na juhudi za wafugaji lakini wanapotaka kuonyesha shughuli zao tunasita kudhamini. Mimi sipati picha kwa kweli.
Mwakani tuhamasiki kwa kudhamini maonyesho ya kilimo (NANE) iwe kampuni, vikundi au binafsi tuelekeze nguvu zetu kwenye kilimo. Kila mmoja wetu anafaidika na kilimo.

No comments: